Kanuni za uchaguzi moto wadau, TLS kutua kortini

Dar es Salaam. Siku nne baada ya baadhi ya wadau kuilalamikia Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) wakidai kutopewa muda wa kutosha kuchambua na kutoa maoni kuhusu kanuni za uchaguzi, Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) kimeeleza kusudio la kuishitaki.

Kanuni hizo ni pamoja na za INEC za mwaka 2024 na Kanuni za Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura za mwaka 2024.

Kanuni hizo zinalenga kutafsiri sheria zilizotungwa na Bunge zinazohusu uchaguzi, ambazo ni Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024 na Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya Mwaka 2024.

Jana, INEC ilizichapisha kanuni hizo kwenye tovuti yake, baada ya kupitishwa Mei 11, 2024 na kuchapishwa kwenye gazeti la Serikali Mei 17, 2024.

Jumapili Mei 19, gazeti hili lilichapisha habari iliyokariri malalamiko ya baadhi ya taasisi, ikiwamo TLS, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Chama cha Wananchi (CUF), ACT-Wazalendo na Chaumma, wakisema hawakupewa muda wa kutosha kutoa maoni.

Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumanne Mei 21 2024, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhani Kailima alisema wadau walishirikishwa.

“Katika vyama vya siasa 19, vyama 16 wamewasilisha maoni, hao ni kina nani ambao hawajawasilisha? Wao kama hawajawasilisha ni hiari yao, hao 16 wamepata muda upi kuwasilisha?” alihoji.

“Wadau 104 tumepokea maoni yao, hao nao wamepata muda upi? Wadau hao wametoa maoni na tumeyafanyia kazi na katika vyama 19, 16 vimetoa maoni yao, hivyo vimepata muda upi?” alihoji Kailima.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo, Kaimu Mkurugenzi wa TLS, Mackphason Mshana amesema wanashauriana na wadau kuangalia namna ya kuishtaki INEC.

“Sisi tulishasema muda haukutosha, hivyo hatukutoa maoni, lakini tunaendelea kuzichambua hizo walizopitisha ili tuonyeshe makosa yake na tuwaambie. Tutawaandikia rasmi maana tuna uwezo wa kufanya hivyo kisheria,” amesema Mshana.

“Wakiona umuhimu wa kuja kukaa na sisi ili kuzifanyia kazi, sawa, lakini wakipinga tuna umuhimu wa kwenda mahakamani, kwa sababu hazijafuata utaratibu unaotakiwa kufuatwa.”

Alisema ukiukwaji huo wa utaratibu ni pamoja na kutowashirikisha kikamilifu wadau.

“Utaratibu haukufuatwa, ikiwamo kushirikisha wadau wote kwa sababu hili suala ni la kitaifa na siyo la tume peke yake. Kama wadau hawakushirikishwa maana yake kuna kanuni za utungwaji wa kanuni zimekiukwa,” amesema.

Mshana amesema, “sasa mtu anakupa siku tatu kupitia kanuni za sheria mbili kwa wakati mmoja halafu baada ya hapo, hamjapewa avenue (nafasi) ya kwenda kutoa maoni, halafu zimeshakuwa approved (zimepitishwa), wewe unaona ni sahihi?

“Sisi tunachosema ni muda, ambao ni sahihi kuanzia siku saba na kuendelea. Huwezi ukatoa siku tatu ukatoa maoni yenye mashiko”.

Mshana alisema katika muda huo wangeweza kutafuta kumbukumbu na kuangalia uzoefu wa nchi nyingine.

“Kuna wakati mnahitaji mtafute wataalamu zaidi wawaambie hili suala limekaaje, sasa huwezi ukapata hivyo vyote ndani ya siku tatu,” amesema.

Amesema japo hakuna mwongozo wa muda maalumu wa kutoa maoni, huwa wanatumia siku saba za Bunge la Jamhuri ya Muungano.

“Mara nyingi tunatumia mwongozo wa Bunge ambao unasema angalau wiki moja, lakini kwa upande wa Serikali hakuna mwongozo wowote na hilo ni kosa lililowekwa kimtindo.

“Suala hili lilikuwa halina haraka hiyo, tangu Sheria ya Tume imesainiwa, mpaka itakapoanza kutumika kwa uchaguzi, bado muda ulikuwepo, hatukuelewa kwa nini muda ulitolewa mfupi kiasi hicho, napo ndipo inapotoa wasiwasi kwa wadau kwa nini zinakimbizwa hivyo, wakati ni jambo la kitaifa,” amesema.

Mkurugenzi wa Uhusiano wa CUF, Mohamed Ngulangwa amesema chama hicho kinatarajia kulitafakari suala hilo kwenye kikao cha Baraza Kuu la chama hicho kijacho.

“Tunatarajia kuwa na Baraza Kuu Juni 3 na 4, 2024 litakalofanyika wilayani Kondoa, Mkoa wa Dodoma, tutajadili suala hilo.”

Amesema kanuni hizo zinakwenda kinyume cha dhamira iliyoonyeshwa na Serikali katika vikao vya kilichokuwa kikosi kazi cha wadau wa demokrasia.

Akizungumzia kanuni hizo, mchambuzi wa masuala ya siasa, Bubelwa Kaiza amesema hazina jipya kwa kuwa hazina masuala yaliyokuwa yakilalamikiwa.

Alitaja kifungu cha 9 (3) kinachozungumzia uhusiano kati ya INEC na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC). “Ungetarajia kuwe na standard cooperation principle (kanuni za ushirikiano), kwa sababu ZEC haijabadilika,” amesema.

Ametaja kifungu cha 11(3) kinachoeleza majukumu ya Kamati ya Usaili, katika uteuzi wa walioomba nafasi za ujumbe akisema:

“Kanuni hazijaweka vigezo, sasa utachambuaje kwamba huyu ahojiwe na huyu asihojiwe? Kwa hiyo, watu wanaweza kuomba wengi halafu wenyewe wakachukua wanaowahitaji kwa vigezo wanavyojua wenyewe, kwa sababu hakuna uwazi, halafu hakuna vigezo vinavyojulikana”.

Kuhusu sekretarieti itakayokuwa na katibu wa tume hiyo katika kifungu cha 12, alisema kanuni haisemi katibu huyo atapatikanaje.  “Kwa sababu ile kamati ya usaili, ina Jaji Mkuu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, ina Jaji Mkuu wa Zanzibar, ina Jaji Mkuu wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora halafu ina mtu aliyeteuliwa na Rais kwa kuzingatia jinsia.

“Sasa wanapokutana wanakuwa na sekretarieti, japo haijawekwa kwenye sheria na wao wanaweka kwenye kanuni, lakini haijulikani atapatikanaje,” amesema.

“Halafu Katibu huyo atateua watumishi wasiopungua watano, sasa atateua kwa mamlaka gani?” amehoji Kaiza.

Kuhusu kamati ya uchunguzi katika ibara ya 14 (1), alisema kanuni haielezi watumishi watapatikanaje.

“Kama ni tume huru kwa nini tena Serikali inapita ndani kwa ndani inahudumia tume? Maana yake uhuru wake haupo,” alisema Kaiza.

Kuhusu elimu ya mpigakura, amesema tume haina watumishi wa kutosha kutoa elimu ya mpigakura, lakini imejipa uwezo wa kudhibiti utoaji wa elimu kwa asasi za kiraia.

“Nadhani inaweza kufeli kwa sababu haionyeshi ushirikiano na watoa elimu ya mpigakura,” amesema Kaiza.

“Kwa mfano kwenye ugawaji wa majimbo, sheria inasema tume itatenga majimbo, lakini ni lazima ruhusa itoke kwa Rais na mfumo mzima, unahusisha mkurugenzi wa halmashauri, mkuu wa mkoa, mkuu wa wilaya, katibu tawala wa mkoa na yule wa wilaya. Kwa hiyo tume inawajibika kwa Rais, hivyo haiwezi kuwa huru,” amesema.

Maoni hayo yameungwa mkono na Wakili Gloria Mafole, akisema suala la wafanyakazi wa tume kuteuliwa linaleta dhana ya upendeleo.

“Kwa sababu mtu anaweza kuteua watu wake anaowajua, hivyo italeta upendeleo na kutokuaminika kwa tume,” amesema.

Kuhusu elimu ya mpigakura, alisema tume imejipa mamlaka ya kuzikataa taasisi za kutoa elimu hiyo, lakini haitoi sababu.

“Ilitakiwa sababu ziwekwe wazi, ili mtu ajue amekataliwa kwa nini. Pia, kanuni hazijaweka muda wa kutoa elimu ya mpigakura, hivyo inaweza kusababisha wananchi kukosa elimu. Kukiwa na muda maalumu, watu watajipanga na itaepusha kura zinazoharibika,” alisema Wakili Mafole.

 “Katika eneo hilo, kanuni zinataka taasisi zipeleke maudhui yao kwa tume, lakini haitoi muda maalumu. Kwa sababu vile vitini vinachapishwa, wanaweza kukurudishia leo, kesho ndiyo unatakiwa uanze kutoa elimu, utajiandaa saa ngapi?” amehoji.

Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga alizungumzia majukumu ya kamati ya usaili katika kifungu cha 8 (5), akisema kanuni haijaweka ulazima wa mafunzo ya jinsia kwa mjumbe au wajumbe wapya.

“Tunapendekeza kuweka sharti hilo kwa kuwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu huachwa nyuma katika michakato ya uchaguzi,” amesema.

Kuhusu elimu ya mpigakura, alitaja ibara ya 22(1)-(5) akigusia idhini ya maudhui yanayotumika kutoa elimu ya mpigakura.

“Tume isiweke vikwazo vyovyote kwa asasi za kiraia katika kutoa elimu kwa wapigakura, ili isionekane tume wanawapangia vitu vya kuongea hizo asasi za kiraia, kwa hiyo ziwe huru katika utoaji huo wa elimu ya mpigakura pasipo kuingiliwa na Tume,” amesema Henga.

Related Posts