Shirika la Madaktari wasio na mipaka la MSF limesema takriban watu 85 wamefariki katika hospitali moja kwenye mji wa El-Fasher huko Darfur tangu mapigano yalipozuka kati ya pande zinazozozana nchini Sudan Mei 10.
Mkuu wa mpango wa dharura wa shirika hilo Claire Nicolet, alisema majeruhi tisa kati ya 60 waliopokelewa katika Hospitali pekee iliyosalia mjini El-Fasher, wamekufa siku ya jumatatu pekee.
Tangu mapigano yalipozuka katika mji mkuu wa jimbo la Darfur Kaskazini, hospitali hiyo imepokea “majeruhi 707” na “85 wameaga dunia”.
Kwa zaidi ya mwaka mmoja, mapigano yamekuwa yakiendelea kati ya jeshi la serikali chini ya Abdel Fattah al-Burhan, na wanamgambo wa RSF wanaoongozwa na Mohamed Hamdan Daglo.
El-Fasher ni mji mkuu pekee katika mkoa wa Darfur, ambao hauko chini ya udhibiti wa RSF na ni kitovu cha misaada ya kiutu katika kanda hiyo iliyo kwenye ukingo wa njaa.UN: Mapigano ya silaha nzito mjini El-Fasher nchini Sudan
Mwezi huu, El-Fasher imekuwa kitovu cha mapambano makali licha ya miito ya mara kwa mara ikiwemo kutoka Umoja wa Mataifa kwa wapiganaji kuuokoa mji huo.
Mashuhuda wameripoti milio ya risasi kutoka pande zote mbili, pamoja na mashambulizi ya anga kutoka kwa jeshi. Wakiwa wamenaswa majumbani mwao kutokana na mapigano hayo, wakaazi wengi hawawezi kustahimili vurugu mitaani ili kuwapeleka wapendwa wao waliojeruhiwa hospitalini.UN: Sudan inakabiliwa na ghasia na uhaba wa misaada
Shirika la MSF linasema majeruhi wanaofika Hospitali ya Kusini wanahudumiwa na “daktari mmoja tu wa upasuaji na kuiweka hiyo” chini ya shinikizo kubwa”. Vita hivyo vimesababisha zaidi ya asilimia 70 ya vituo vya afya kote nchini kufungwa na vile vilivyosalia vinatoa huduma katika mazingira duni.
Nicolet ameongeza kuwa hospitali hiyo ya kusini imesalia na vifaa vya siku 10 tu, na kuzitaka pande zinazopigana kuruhusu upelekwaji wa vifaa vya matibabu.WFP yafikisha msaada wa chakula Darfur
Tangu vita ilipoanza maelfu ya watu wameuawa, ikiwemo karibu watu 15,000 katika mji mmoja wa Darfur Magharibi, kulingana na wataalam wa Umoja wa Mataifa.
Takriban watu milioni tisa wamelazimika kukimbia makazi. Mwishoni mwa mwezi Aprili, Darfur Kaskazini pekee ilipokea zaidi ya watu nusu milioni waliokimbia makazi yao mwaka jana, kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa.