Ni mwanzo wa mwisho wa uongozi wa wazee Afrika?

Kama kipimo cha ujana ni chini ya umri wa miaka 50, basi Afrika ilikombolewa na vijana. Ukianzia kwa  Kwame Nkrumah, aliyeiwezesha Ghana kupata uhuru akiwa na umri wa miaka 47, hadi Mwalimu Julius Nyerere, aliyeiondoa Tanganyika kutoka kwa wakoloni Uingereza, akiwa na umri wa miaka 39.

Ahmed Sekou Toure, aliyeipa Guinea uhuru, akiwa na umri wa miaka 36, halafu Kenneth Kaunda, aliyewang’oa Waingereza Zambia, alipokuwa na umri wa miaka 40. Kisha, Ahmadou Ahidjo, ambaye aliiwezesha Cameroon kuwa huru, umri wake ukisoma miaka 35.

Gambia, Dawda Jawara, aliiwezesha nchi hiyo kuwa taifa huru alipokuwa na umri wa miaka 40. Patrice Lumumba, alifanikisha kuifanya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kuwa nchi huru, siku mbili kabla hajatimiza umri wa miaka 35. Yupo Seretse Khama, aliyeipa Botswana uhuru akiwa na umri wa miaka 44.

Ni muhtasari, kuonyesha asili ya uhuru wa Afrika. Zipo nchi nyingi tu ambazo uhuru wake uliwezeshwa na watu wa makamo mpaka wazee. Hata hivyo, lengo ni kudhihirisha kuwa Afrika ilipokuwa inajichomoa kwenye makucha ya wakoloni, vijana ndiyo walikuwa mstari wa mbele.

Jambo moja linafanana sehemu nyingi Afrika; vijana walioshika uongozi kutoka kwa wakoloni, wengi walikaa madarakani hadi kupitiliza, wengine walifikwa na mauti wakiwa bado wanaongoza ofisi kuu za nchi zao. Sekou Toure, shujaa wa uhuru wa Guinea akiwa na umri wa miaka 36, alikufa akiwa madarakani, Machi 26, 1984, alipokuwa na umri wa miaka 62.

Kaunda Zambia, aliingia ofisini akiwa na umri wa miaka 40, akaondoka miaka yake ikisoma 68. Mwalimu Nyerere, aliyeingia madarakani na umri wa miaka 39, aliachia nchi alipokuwa na umri wa miaka 63. Hakuna kijana aliyewezesha taifa lake lipate uhuru, aliyeachia madaraka kwa hiari ndani ya miaka 10.

Mei 10, 2024, Mahamat Deby, akiwa na umri wa miaka 40, alikula kiapo kuiongoza Chad. Deby, alishinda Uchaguzi wa Urais Chad, uliofanyika Mei 6, 2024. Awali, Deby, alianza kuiongoza Chad kijeshi akiwa na umri wa miaka 37, kufuatia kifo cha baba yake, Idriss Deby, aliyefia madarakani Aprili 20, 2021.

Mwezi mmoja kabla, Wasenegali waliushangaza ulimwengu, walipomchagua Basirou Faye, mwenye umri wa miaka 44, kuwa rais wa nchi yao. Haikuwa mara ya kwanza Senegal kuchagua rais kijana, kwani hata Rais wa Pili wa nchi hiyo, Abdou Diouf, aliingia ofisini mwaka 1981, alipokuwa na umri wa miaka 45.

Maajabu ya Faye, ni jinsi alivyochaguliwa kuwa rais katika zama za sasa, ambazo vijana wa zamani waliozeekea madarakani, hawataki kuachia madaraka. Halafu, wazee wanaopisha, wanakabidhi usukani kwa wazee wenzao, wakidai vijana hawajakomaa. Wakati vijana ndiyo walioipa uhuru Afrika kwa sehemu kubwa.

Yoweri Museveni, aliyekamata dola ya Uganda alipokuwa na umri wa miaka 45, hivi sasa akielekea kutimiza umri wa miaka 80, haamini kama kijana wa leo aliyeishi miaka 45 duniani, ana akili, uwezo na maarifa ya kuongoza nchi hiyo kwa mafanikio.

Kijana anayeshika madaraka leo, atatambia ujana wake. Miaka inayofuata, hatakuwa kijana tena, lakini atang’ang’ania madaraka. Viongozi wengi vijana hudhani wao walikuwa maalumu mno kwenye nyakati zao, ndiyo maana hudharau vijana wa kizazi kipya, kwa kuona hawana uwezo wa kuongoza. Kikwazo cha vijana wa sasa ni vijana wa zamani waliopata nafasi.

Hata hivyo, zama zinabadilika. Rais wa Cameroon, Paul Biya, 91, anajikuta anapakana na Chad, ambayo rais wake ni kijana mwenye umri wa miaka 40. Hata Biya mwenyewe, aliingia ofisini akiwa na umri wa miaka 49. Ameendelea kung’ang’ania madaraka licha ya umri mkubwa alionao.

Pengine vijana wanaona ni muda mwafaka kuchukua dola, ikibidi hata kwa nguvu ya jeshi. Burkina Faso, sasa inaongozwa na Ibrahim Traore, mwenye umri wa miaka 36. Traore, alishika dola tangu Septemba 30, 2022 kwa mapinduzi ya uasi wa kijeshi.

Hali ipo hivyo hata Mali. Nchi hiyo inaongozwa na Assimi Goita, mwenye umri wa miaka 40. Goita, aliongoza mapinduzi mwaka 2021. Wapo watu wanasema makoloni ya zamani ya Ufaransa, yamekithiri mapinduzi, hawashangai jinsi vijana ambavyo wamekuwa na kasi ya kuongoza mataifa yao Afrika, hususan kwenye nchi zenye kuzungumza lugha ya Kifaransa.

Muktadha unapoegemea kwenye nchi zenye kuzungumza lugha ya Kifaransa, unafika mpaka Guinea, ambayo kiongozi wake ni Mamady Doumbouya, ambaye ana umri wa miaka 44. Doumbya, aliingia ofisini mwaka 2021 akiwa na umri wa miaka 41 kwa mapinduzi ya kijeshi.

Linaweza kuwepo swali je, vuguvugu hili la vijana kuingia madarakani kwa kasi, linashabihiana na lile la Samuel Doe, Liberia, aliyeingia madarakani kwa mapinduzi laini ya kijeshi, Aprili 12, 1980, akiwa na umri wa miaka 28, au Valentine Strasser, aliyejitwalia dola ya Sierra Leone, alipokuwa na umri wa miaka 25.

Doe “Master Seargent”, aliondoka madarakani baada ya kutimiza miaka 10 kwa aibu, mateso hadi kifo. Alikuwa na miaka 39, Doe alipoburuzwa na gari barabarani, kisha kukatwa masikio akirekodiwa video. Strasser, kama alivyoingia kijana, ndivyo alivyoondoka. Alitimuliwa ofisini akiwa na umri wa miaka 29.

Je, vuguvugu la sasa la vijana kuingia madarakani, linashabihiana na zama za uhuru? Vijana wanaopata fursa ya kuongoza sasa, utafika muda wataachia madaraka kikatiba, au wataanza hila, mithili ya vijana wa zamani waliowezesha Afrika kupata uhuru kwa sehemu kubwa?

Hajasahaulika Pierre Nkurunzinza, aliyeingia madarakani Burundi akiwa na umri wa miaka 40. Alipotimiza umri wa miaka 50, akiwa ameshakaa ofisini kwa mihula miwili yenye jumla ya miaka 10, aligoma kuachia ngazi. Hata alipokamilisha mihula mitatu, alibadili Katiba ili yeye abaki kuwa mtawala, huku rais mpya akiwa kivuli chake. Mungu alimchukua Nkurunziza siku chache baada ya Rais Evariste Ndayishimiye, kushinda kiti cha urais.

Hata DRC, Joseph Kabila, aliingia madarakani akiwa na umri wa miaka 29. Alikaa ofisini kwa miaka 18, akaachia nchi baada ya sarakasi nyingi, alipokuwa na umri wa miaka 47. Hivi sasa, Kabila akiwa na umri wa 52, taarifa za uhakika ni kwamba anajipanga kurejea madarakani baada ya Rais Felix Tshisekedi, kumaliza mihula miwili.

Adui wa vijana ni vijana wa zamani au ule utamu wa madaraka? Afrika, kila anayeonja akiwa na umri mdogo, hutamani kuendelea. Upo mfano Madagascar. Andy Rajoelina, alishinda kwa mara ya kwanza urais, alipokuwa na umri wa miaka 34. Dunia iliimba jina lake kwa jinsi alivyoshinda kiti katika umri mdogo.

Mei 30, 2024, Rajoelina atatimiza umri wa miaka 50. Ndiye rais aliye madarakani. Mwaka 2014, alikaa pembeni, kisha mwaka 2019 akarejea kitini. Bado yupo. Mwaka 2028, Madagascar itafanya uchaguzi mwingine wa urais. Bila shaka, Rajoelina akiwa hai, atagombea tena. Wakati huo, atakuwa na umri wa miaka 54. Ndiyo maana vijana wanatumia jeshi kufanya mapinduzi, maana wanajua adui wa vijana ni vijana waliopata madaraka kipindi cha ujana wao.

Related Posts