MKOA wa Pwani umekuwa sehemu ya kuchagiza mabadiliko hasi ya tabia nchi , pamoja na uharibifu wa mazingira, kutokana na uwepo wa soko kubwa la mkaa unaotumika zaidi Jiji la Dar es Salaam.
Hayo aliyaeleza Kaimu Katibu Tawala Mkoani Pwani, upande wa Menejiment,Ukaguzi na Ufuatiliaji, Nsajigwa George alipokuwa akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Pwani kuzindua Mradi Jumuishi wa kuhifadhi misitu na kuboresha mnyororo wa thamani ya mkaa, uliofanyika Bagamoyo.
Mradi huo unaratibiwa kwa ushirikiano kati ya Taasisi ya Huduma za Nishati Endelevu ( TaTEDO-SESO) na Jumuiko la maliasili Tanzania (TNRF) kwa ufadhili wa Jumuiya ya Ulaya.
“Mkaa ni moja ya chanzo kikuu cha kipato kwa jamii mkoa wa Pwani,kwa kiasi kikubwa uchomaji mkaa ni holela, Hali hii inasababisha mkoa huu kuwa sehemu ya kuchagiza uharibifu wa mazingira.” alieleza.
Nsajigwa alielezea kuwa, kwa mujibu wa takwimu za bank ya Dunia ,mwaka 2010-2013 inaonyesha Tanzania ilikuwa inazalisha tani milioni moja ya mkaa na asilimia 50 ikitumika Dar es Salaam.
“Kwa takwimu za sasa uzalishaji ni milioni 2.5 ambapo asilimia 60 inatumika Dar es Salaam, ongezeko hili Kila mtanzania anatakiwa kubadilika na kuwa na mtazamo chanya wa kuhifadhi misitu na mazingira kwa ustawi wa Nchi, Afrika na Dunia ” alifafanua Nsajigwa.
Vilevile Nsajigwa aliongeza kwamba, kwa sasa Tanzania ina watu zaidi ya milioni 61 na inakadiriwa ikifikia 2050 kutakuwa na watu milioni 129.39 kwa namna hii mahitaji yataongezeka maradufu hali itakayoendelea kuchagiza uharibifu wa mazingira,misitu mara dufu “
Alisema,kwa ujumla mabadiliko ya tabia nchi yamekuwa tishio la Dunia kwa sasa ambayo yanachangiwa na shughuli za kibinadamu.
Kadhalika alieleza, mradi huo utakuwa tiba ama mwarubaini dhidi ya ukataji miti na uharibifu wa mazingira katika mikoa vinara inayoongoza kwa uharibifu wa mazingira na Taifa kijumla.
Nsajigwa alisema, Rais Samia Suluhu Hassan ,kama kinara na champion wa kuhimiza nishati safi ya kupikia Afrika, ameibeba agenda hiyo ili watanzania waondokane na matumizi ya isiyo salama .
Nae Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Huduma ya Nishati Endelevu (TaTEDO -SESO), Jansen Shuma , alieleza anaamini mradi huo utakuwa mwanzo wa maboresho na mabadiliko makubwa katika matumizi ya nishati mbadala.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Jumuiko la Maliasili Tanzania (TNRF) Zakaria Faustine alipongeza juhudi zilizofanywa na wadau wote hadi kufikia hatua ya uzinduzi.