WADAU WA HUDUMA ZA WARAIBU (MAT ) MKOANI TANGA WAKUTANA KUJADILI MAENDELEO YA UTOAJI WA HUDUMA HIZO


Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga Imani Clemence akizungumza wakati wa kikao cha wadau wa huduma za waraibu (MAT) mkoani Tanga kimefanyika Jijini hapa kwa ajili ya kujadili maendeleo ya utoaji wa huduma hizo.

Mkurugenzi Mshirika wa Huduma za Jamii –Huduma za Kinga (THPS) Dkt Appolinary Bukuku akizungumza katika kikao hicho




Afisa kutoka Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya Kanda ya Kaskazini Sara Ndaba akizungumza jambo wakati wa kikao hicho

Na Oscar Assenga, TANGA.

KIKAO cha wadau wa huduma za waraibu (MAT) mkoani Tanga kimefanyika Jijini hapa kwa ajili ya kujadili maendeleo ya utoaji wa huduma hizo.

Kikao hiki kilihudhuriwa na wawakilishi kutoka Kamati ya Usalama ya Mkoa, Timu za Menejimenti ya Afya za Mkoa na Halmashauri (R/CHMT), wawakilishi kutoka Asasi za Kiraia, wanufaika wa huduma za MAT, watoa huduma za afya, na maafisa wa Shirika la Tanzania Health Promotion Support (THPS).

Akizungumza wakati akifungua kikao hicho, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Bw. Imani Clemence alisema Serikali kushirikiana na wadau mbalimbali, wakiwemo THPS imeweka nguvu kubwa katika kuboresha huduma za waraibu kuhakikisha wanapata huduma bora ili afya zao ziweze kuimarika na wafikie hali ambayo wanaweza kuishi maisha ya kawaida na kushiriki katika kujenga uchumi.

Bw. Clemence alisema hadi sasa waraibu 1,094 wamejiandikisha kwa ajili ya kuanza huduma mkoani hapa, lakini 683 pekee ndio wanaendelea na huduma.
“Kuna waliohitimu, waliohama, waliopotea na wengine waliokufa”, alisema Bw. Clemence.

Bw. Clemence alishukuru Shirika la THPS ambalo limetoa mchango mkubwa sana katika kutoa kuduma za MAT, matunzo na tiba kwa WAVIU na huduma za Kufua Kikuu, kupitia mradi wa Afya Hatua unaofadhiliwa na Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI (PEPFAR) kupitia Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Marekani (U.S. CDC).

“Tutaendelea kuwapa ushirikino katika miradi inayoendelea kutekelezwa mkoani Tanga wakati wote mtakapokuwa mkiitaji na niwashukuru wadau wote tunaoshirikiana nao kwenye pambano dhidi ya dawa za kulevya”Alisema

Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi wa THPS, Dkt Appolinary Bukuku alisema Shirika la THPS litaendelea kuchangia katika juhudi za Serikali ili watanzania wote waweze kufikiwa na huduma bora za afya.

“Tunatambua kuna watu wameingia katika uraibu, lakini huko nyuma walikuwa na uwezo wa kufanya kazi kama sisi lakini kutokana na athari walizokutana nazo wameshindwa kufanya kazi na kutengwa na jamii. Huduma hizi zinazolewa na Serikali na wadau zitawasdia kuwawezesha kurudi katika Maisha yao ya awali”, alisema

Naye kwa upande wake Afisa kutoka Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya Kanda ya Kaskazini Sara Ndaba alisema kwamba wanalishukuru Shirika la la (THPS) kwa kuandaa kikao hicho cha wadau kwani wamekuwa wakiwasadia kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya.

Alisema katika kikao hicho kimewakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa Dini,Jeshi la Polisi,Jeshi Magereza na Wizara ya afya wote wanapambana kwenye vita dhidi ya dawa za kulevya na mkoa umethirika na dawa za kulevya.

Hata hivyo alisema kwamba uwepo wao utasaidia kukabiliana na tatizo hilo na Tanga ikaondokana na tatizo la dawa za kulevya kwa maana hali bado sio shwari kutokana na kwamba kituo cha MAT kinahudumia waraibu zaidi watu 683 kila siku mpaka sasa kutoka kwa Asasi za kiraia ambazo zimekuwa zikiwaibua na kuwapeleka kwenye kituo .

Wapokea huduma za MAT nao walipata fursa ya kuzungumza kuhusu maisha yao ya uraibu na jinsi huduma wanazopatiwa zinavowasaidia kurudi katika maisha ya kawaida. Hadithi zao zilikuwa ukumbusho wa umuhimu wa kuendelea kusaidia na kupanua huduma za MAT katika mkoa wa Tanga.

Ushirikiano kati ya wadau mbalimbali na juhudi za pamoja zinahitajika katika kushughulikia matumizi mabaya ya dawa na uraibu kwa ufanisi.

Related Posts