Serikali imesema hadi sasa watumishi wa umma 25,039 wamehamia Makao Makuu ya Nchi Jijini Dodoma pamoja na Taasisi 65 ambapo inaendelea na mpango kazi wa ujenzi wa Awamu ya Pili wa majengo ya Ofisi za Wizara na Taasisi unaotarajiwa kukamilika mwaka 2025.
Hayo yalisemwa leo tarehe 21 Mei, 2024 Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. Ummy Nderiananga wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Bahi, Mhe. Keneth Nollo aliyehoji ni lini mpango wa kuhamia Dodoma utakamilika na ni taasisi ngapi zimeshahamia mpaka sasa.
Mhe. Nderiananga alieleza kwamba Mpango wa kuhamisha Makao Makuu ya Serikali kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma ulianza rasmi mwaka 2016.
“Hadi sasa, jumla ya watumishi 25,039 kutoka Serikali kuu, Bunge, Mahakama, Vyombo vya Ulinzi na Usalama, pamoja na Taasisi 65 wameshahamia na wanaendelea kutekeleza majukumu yao wakiwa Dodoma. Pia Serikali inatarajia kukamilisha mpango wake wa kuhamia Dodoma kwa kuzingatia Mpango kazi Maalum wa ujenzi wa Awamu ya Pili ya ujenzi wa ofisi hizo,”Alisema Mhe. Nderiananga.
Kuhusu ujenzi wa nyumba za watumishi alibainisha kuwa Serikali ilianza ujenzi wa makazi rasmi ya viongozi kuanzia mwaka 2021/2022 kupitia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ambapo nyumba 20 zilijengwa wakati hadi kufikia Mwezi Septemba mwaka 2023 nyumba za watumishi 150 ikiwemo nyumba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Kwa sasa tuko kwenye zoezi la kupanga eneo ambalo tumelitoa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za viongozi wa Serikali na watumishi wa umma tutakuwa na Ekari 4654 kati ya Mji wa Serikali Mtumba na Ikulu,”Alieleza Mhe. Nderiananga.
Aidha, aliwahakikishia Watanzania kwamba Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea na mpango wake wa kuendeleza Mji wa Serikali- Mtumba kama ilivyokusudiwa.