Askari Kinapa anayedaiwa kumuua raia kwa risasi apandishwa kortini

Moshi. Gabriel Chacha Chokela, ambaye ni askari wa Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (Kinapa), amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Moshi, akikabiliwa na kesi ya mauaji ya mwananchi wa kiijiji cha Komela, Octavian Temba (38).

Temba ambaye anadaiwa kuuawa kwa kupigwa risasi Mei 9, mwaka huu akiwa ndani ya msitu wa Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro akikata majani ya mifugo wake, alizikwa kijijini hapo Mei 12, mwaka huu, huku akiacha watoto wadogo wanne na mke mmoja.

Chacha ambaye anakabiliwa na kesi hiyo ya mauaji namba 13163 ya mwaka 2024, alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Mei 17 mwaka huu, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Rehema Olambo.

Hata hivyo, askari huyo ambaye hakuruhusiwa kujibu chochote mahakamani hapo, kesi yake imepangwa kutajwa tena Mei 31, mwaka huu.

Mei 9, mwa huu kulipotokea tukio hilo la mauaji, Kamanda wa polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, alisema Jeshi hilo linawashikilia  askari wawili wa  hifadhi hiyo pamoja na Mgambo mmoja kwa kudaiwa kuhusika na mauaji hayo.

Baada ya kutokea mauaji hayo, wananchi zaidi ya 200 waliandamana mpaka geti la Marangu kupinga mauaji yaliyofanywa na askari hao, hali ambayo ilisababisha vurugu na kuharibu miundo mbinu ya barabara pamoja mabomba ya maji.

Related Posts