Liwale. Mawasiliano yaliyokatika kati ya wilaya za Kilwa Masoko na Liwale mkoani Lindi yamerejeshwa baada ya ukarabati wa daraja la muda katika Mto Zinga.
Kukatika kwa daraja hilo ambalo pia linaunganisha vijiji vya Zinga na Miguruwe mbali ya kuathiri shughuli za usafirishaji, liliathiri masomo kwa wanafunzi waliolazimika kupita ndani ya maji ili kuifikia shule.
Mawasiliano yalikatika baada ya daraja kusombwa na maji yaliyotokana na mvua kubwa iliyoambatana na upepo uliosababishwa na Kimbunga Hidaya kilichotokea Mei 3 na 4, mwaka huu.
Ili kuvuka eneo hilo, iliwalazimu wavukaji kuvua viatu na kuhakikisha kama ni gauni linapandishwa juu sawa na wavaaji wa suruali ili kuvuka. Wenye mizigo waliomba usaidizi ili kuvushwa.
Akizungumza na Mwananchi, Mary Mwela, mkazi wa Kijiji cha Miguruwe amesema kuharibika kwa daraja kulisababisha watoto kushindwa kwenda shule kutokana na kulazimika kupita kwenye maji.
“Watu wa Miguruwe walikuwa wa Miguruwe wa Njinjo walikuwa wa Njinjo, watoto wakitaka kwenda shule ni lazima tuwasindikize kuwavusha hapa mtoni au maji yakiwa mengi tunawazuia wasiende,” amesema Mwela.
Khadija Nassor, mwanafunzi wa darasa la pili amesema alilazimika kumsubiri kaka yake wa darasa la sita ili amsaidie kuvuka.
“Tukifika hapa ananibeba, tukivuka naendelea kutembea, mvua ikiwa kubwa hatuendi shule,” amesema Khadija.
Mjumbe wa Halmashauri ya Kijiji cha Miguruwe, Mwajuma Kassim amesema walikabiliwa na changamoto ya kuzifikia huduma muhimu zikiwemo za afya kwa mama na mtoto hasa walipotakiwa kwenda Hospitali ya Wilaya ya Kilwa Kivinje.
“Tunashukuru tumepata daraja la muda, tunaiomba Serikali ihakikishe inatujengea daraja la kudumu ili maisha yetu yaendelee kama kawaida,” amesema Mwajuma.
Dereva wa bodaboda, Fadhili Ngulile amesema usafirishaji ulikuwa mgumu awali kutokana na kuongeza gharama za uendeshaji kwa wamiliki.
Kutokana na hilo, amesema walilazimika kutoa fedha mara mbili zaidi ili kufikisha mizigo katika vijiji vilivyokusudiwa hasa vilivyo njiani kueleke Wilaya ya Liwale.
“Mfanyabiashara akija na mizigo kutoka Kilwa akifika hapa analazimika kushusha kwenye gari ili ivushwe na pikipiki kwenda ng’ambo ya pili au sehemu anayotaka kufika ni gharama nyingine. Tunashukuru Serikali imetuona na kutujengea daraja hili la muda,” amesema Fadhili.
Dereva wa gari la abiria kati ya Dar es Salaam na Zinga, Abdul Sadick amesema kwa kawaida nauli ilikiwa Sh25,000 kati ya Dar es Salaam hadi wanapoelekea lakini daraja lilipoharibika gharama iliongezeka kutokana na abiria kulazimika kushuka ili waweze kupanda bodaboda.
“Sisi tulikuwa tukifika hapa Njinjo safari mwisho, abiria wanashuka wanavuka maji na kupanda pikipiki kwa kuanzisha Sh15,000 hadi Sh25,000 kufika Zinga kutoka hapa, hali hii itakwisha na italeta ahueni kwao,” amesema Sadick.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Miguruwe, Hemed Kingwande amesema hofu ya wananchi ilikuwa mazao yao kwa msimu huu kukosa soko kwa kuwa ufuta mara zote huuzwa kwa mnada.
“Soko kubwa la mnada liko Nangurukuru, wakulima walikuwa wameingiwa wasiwasi wakidhani mwaka huu hawatafanya mnada wa zao hilo,” amesema Kingwande.
Akizungumzia kilichofanyika, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Lindi, Emil Zengo amesema kimbunga Hidaya kilipopita maji yaliongezeka na kupita juu ya daraja.
“Daraja lilisukumwa kabisa, kusogea pembeni na kuta zake kubomolewa, kimbunga kilisababisha athari katika maeneo mengine pia ya barabara zetu, ikiwamo Barabara Kuu ya Dar es Salaam kuja Lindi hadi Mtwara,” amesema Zengo.
Kukatika kwa barabara kulisababisha Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa kutoa maelekezo ya saa 72 kwa Tanroads kufanya marekebisho.
Amesema kwa sasa eneo hilo limekamilika na barabara ya kutoka Liwale hadi Nangurukulu inapitika, matengenezo madogo madogo yakiendelea kwa baadhi ya maeneo.
Kimbunga Hidaya kilisababisha zaidi ya madaraja manne kukatika yakiwamo ya Somanga, Mikereng’ende, na la Mto Matandu, huku baadhi ya vijiji vikizingirwa na maji.
Anna Nnko, msimamizi wa Barabara ya Kilwa Masoko-Nangurukuru-Liwale, amesema mbali na daraja hilo, ipo sehemu ya barabara hiyo ilimegwa na maji yaliyosababishwa na mvua kubwa za El-Nino.
Amesema Tanroads ililazimika kuihamishia upande mwingine ili shughuli za kiuchumi ziweze kuendelea.