Chongolo, RPC wang’aka ubakaji watoto Songwe, ushirikina watajwa

MKUU wa mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo kwa kushirikiana na kamati ya usalama ya mkoa, ametangaza vita kwa watu wanaoendekeza vitendo vya ubakaji na ukatili kwa watoto ikiwa ni pamoja na mauaji yanayotokana na wivu wa kimapenzi na imani za kishirikina wanazoshauriwa na baadhi ya waganga wa kienyeji. Anaripoti Ibrahim Yassin Songwe… (endelea).

Chongolo ametoa onyo hilo jana Jumanne wakati akizungumza na wananchi wilayani Momba ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake mkoani humo kukagua miradi ya maendeleo.

Amesema katika mkoa huo kumekithiri matukio ya ajabiu ikiwamo baadhi ya wananchi wanaoshindwa kupanga mikakati ya kubuni njia sahihi za kutafuta fedha badala yake kwenda kwa waganga wa kienyeji ambao wanawaeleza kuwa ili wapate mali, wabake watoto.

”HIvi hao wanganga wanaotoa maelezo hayo kwa wateja wao, wenyewe hali zao zipoje? ninyi wananchi acheni kudanganywa, eti unaambiwa ili upate mavuno mengi au dhahabu nyingi basi umbake mtoto tena wa kumzaa na wewe unakubali alafu matokeo yake unaendelea kuwa masikini… acheni imani hiyo ni potofu,” amesema Chongolo.

Hata hivyo, Chongolo amesema yeye na kamati yake wamejipanga kuhakikisha wanashughulikia wote wanaotenda unyama huo.

Daniel Chongolo

Aidha, akizungumzia matukio hayo, Kamanda wa polisi mkoani Songwe, Augostino Senga amesema katika siku za hivi karibuni, mtoto mwenye umri wa miaka  miwili alibakwa na kutelekezwa kwenye shamba la mahindi wilayani Songwe.

Amesema baada ya jeshi la polisi kupata taraifa walienda eneo hilo na kukuta mtoto ameshafariki kutokana na maumivu na njaa.

Amesema mbali na tukio hilo pia kuna baba anatuhumiwa kumbaka mtoto wake wa kumzaa kwa imani kamba atapata mafanikio kimaisha.

”Nina muda wa mwezi mmoja na nusu toka niletwe mkoa huu wa Songwe, nimekuta baadhi ya matukio ya aina hii yametokea. Niwahakikishie wote mnaoendekeza hali hii hamtobaki salama. Wahusika wote tutawakamata… nawasihi ndugu zangu acheni watoto wasome, msijiingize kwenye matukio hayo,” amesema Kamanda Senga.

Related Posts