Tasaf yatoa matumaini wanufaika wapya

Dar es Salaam. Familia maskini ambazo hazikupata nafasi ya kuingia katika mpango wa kuwezesha kaya hizo kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf),  sasa zitawezeshwa pindi awamu mpya itakapotangazwa na Serikali.

Tasaf imesema kila kinachofanyika kinakwenda kwa utaratibu na kuzingatia miongozo.

Ofisa Maendeleo ya Jamii, Nellusigwa Mwakigonja amesema hayo hivi karibuni, wakati akizungumza na wananchi wa Mohongay wilayani Mbulu katika ziara ya watendaji wa Tasaf na Benki Kuu ya Dunia (WB).

“Tasaf hii ya kunusuru kaya maskini, tulikuwa na awamu ya kwanza iliisha mwaka 2020, tupo awamu ya pili iliyopo ukingoni, tuwe na subira inaweza tukapata fursa kwenda awamu ya tatu au Serikali kuja mpango tofauti utakaogusa maisha ya wato,” amesema Mwakigonja.

 “Mpango huu wa Tasaf umeanza muda mrefu kidogo na ulikuwa unakwenda kwa awamu na kaya maskini bado zinatakiwa zifikiwe, je viongozi wa Tasaf na Benki ya Dunia mna mpango gani kuzisaidia ili kupata unafuu wa maisha,” amehoji Ibrahimu Dipobadi mwanakijiji wa Mohongay.

Hata hivyo, katika majibu yake Mwakigonja amesema Serikali inatambua katika kaya za Watanzania umaskini unaweza kutokea wakati wowote, hivyo wakati wa awamu ya kwanza baadhi yao hawakuwa na sifa za kuingia kwenye mpango, lakini hivi sasa wana vigezo.

“Tunatambua mpango huu, unatekelezwa kwa awamu, kuna watu waliingia mwaka 2015, walitakiwa kukaa kwa miaka mitatu ili kuwapisha wengine, lakini baada ya utekelezaji wa miaka ilionekana walengwa bado hawajanufaika vema hata leo hii nani yupo tayari kutoka.

“Lakini wakati tunaibua kaya maskini, mikutano ilifanyika kuna kaya zilikataa wakidai ni Freemason na wengine walisema fedha za kampeni leo hii wamegeuka wanataka kuingia kwenye mchakato,” amesema Mwakigonja.

Katika ziara hiyo wananchi walihudhuria mkutano na wawakilishi wa Benki ya Dunia waliokwenda kukagua shughuli mbalimbali za utekelezaji wa miradi ya Tasaf inayolenga kuwasaidia wananchi kujikwamua na umaskini.

Mtaalamu wa Mazingira Tasaf, Amos Mkude wa Tasaf amesema wameshirikiana na WB kuangalia shughuli za utekelezaji wa miradi ya Tasaf, ikiwamo mafanikio na changamoto, sambamba na kushauri namna ya kushauri maeneo yanayotakiwa kuboreshwa zaidi.

“Katika Mkoa wa Manyara tumetembelea vijijini vinne vya wilaya za Mbulu na Hanang, tumepata nafasi ya kuzungumza na watalaamu wa ngazi ya halmashauri,” amesema Mkude.

Mbali na Mkude, mtaalamu mwingine wa mazingira wa WB, Edina Kashangaki amesema amefurahishwa na utekelezaji wa miradi ya Tasaf hasa kwa wananchi kujiongeza katika shughuli za kujiletea maendeleo.

“Kuna mzee mmoja alituambia kulikuwa na mpango wa kujenga bwawa la matumizi ya umma, akachukua ujuzi na kuupeleka shambani kwake kutengeneza bwawa dogo la kumwagilia miwa ambayo ikistawi anaweza kupata faida ya milioni moja hadi mbili baada ya kuvuna,” amesema.

Roselyn Kaihula wa WB amesema wanufaika wanashukuru miradi ya Tasaf kwa sababu inaboresha maisha licha ya kupata fedha, wanapata ujuzi kupitia miradi inayotekeleza katika maeneo yao.

“Kuna maeneo mengine tabia za wanakijiji zimebadilika, wengine walikuwa wanalewa, wameacha kutokana ushauri wanaopewa na wataalamu wa Tasaf kuhusu fedha. Ila katika vijiji vingine kuna kazi kubwa ya kufanya kutokana na utamaduni tofauti,” amesema Kaihula.

Related Posts