PPAA kuanza kutumia kanuni za rufani Julai 2024

Na Mwandishi Wetu

Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) imejipanga kuanza kutumia Kanuni za Rufaa za Ununuzi wa Umma za mwaka 2024 rasmi kuanzia Julai 01, 2024.

Hayo yalibainishwa na Katibu Mtendaji wa PPAA, James Sando Jijini Dodoma wakati wa kikao kazi cha kupokea maoni ya uandaaji wa Kanuni za Rufaa za Ununuzi wa Umma za Mwaka 2024 ili kuiwezesha Sheria ya Ununuzi Umma ya Mwaka 2023

Sando amesema Sheria Na.10 ya Ununuzi wa Umma ilitungwa na kupitishwa na Bunge Septemba 2023 ambapo ili iweze kutumika kwa ufanisi inategemea kanuni za ununuzi ambazo zipo katika hatua mbalimbali na zitakamilika na kuanza kutumika rasmi katika mwaka ujao wa fedha.

“Sheria ipo tayari lakini haiwezi kutumika bila kuwa na kanuni ndio maana tuko hapa kwa ajili ya kupokea maoni ya wadau wa ununuzi kuhusu Kanuni za Rufaa za Ununuzi wa Umma za Mwaka 2024 ili kuiwezesha Sheria ya Ununuzi Umma ya Mwaka 2023,”amesema Sando.

Sando ameeleza kuwa anaamini sheria hizo, zinakwenda kupunguza changamoto kwenye rufani za manunuzi zilizokuwepo awali ambapo zilikuwa zikilalamikiwa na wazabuni.

Awali Kamishna wa Sera ya Ununuzi wa Umma, kutoka Wizara ya Fedha, Dk. Frederick Mwakibinga ambaye alimwakilisha Mgeni Rasmi – Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Jenifa Omolo, amesema Serikali imefanya maboresho makubwa katika sheria hizo, hivyo watu watarajie mageuzi makubwa.

Dk. Mwakibinga amesema baada ya kanuni kukamilika zitasaidia wananchi hususani wazabuni na wadau wa ununuzi kwenda kutumia kanuni ambazo zimekamilika na kuboreshwa na kuisaidia Serikali kupata thamani halisi ya fedha katika ununuzi wa umma.

Amefafanua zaidi kuhusu mabadiliko ya sheria ambapo amesema Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023 imeboresha masuala mbalimbali ikiwepo kupunguzwa kwa muda wa kushughulikia malalamiko na rufaa zinazotokana na michakato ya ununuzi wa umma.

“Mfano, muda wa siku saba za kazi kwa ajili ya kusubiri malalamiko ya wazabuni (cool off period) kabla ya kutoa tuzo umepunguzwa na kuwa siku tano za kazi. Muda huo hautajumuisha njia za ununuzi ambazo hazihitaji ushindani kama vile ‘single source minor value procurement na shopping, kadhalika muda wa Afisa Masuuli kushughulikia malalamiko ya zabuni umepunguzwa kutoka siku saba za kazi hadi siku tano za kazi pale ambapo hataunda jopo,”amesema Dk. Mwakibinga.

Aidha, Dk. Mwakibinga ameongeza kuwa kutokana na maboresho hayo endapo Ofisa Masuuli ataunda jopo la mapitio ya malalamiko basi atakuwa na siku saba za kazi na atatakiwa kuwajulisha washiriki wote wa zabuni juu ya uundwaji wa jopo hilo. Sambamba na hilo muda wa PPAA kushughulikia malalamiko au rufaa umepunguzwa kutoka siku arobaini na tano hadi siku arobaini.

“Hivyo ili kuwezesha utekelezaji wa sheria mpya ya ununuzi wa umma ya mwaka 2023, PPAA ipo katika mchakato wa kuandaa kanuni za rufaa za ununuzi wa umma za mwaka 2024 ambapo pamoja na mambo mengine, kanuni hizo zitatoa wigo mpana wa kuwasilisha malalamiko. Mabadiliko hayo yatawapa wazabuni fursa ya kushindana kwa haki na uwazi katika zabuni mbalimbali,” amesema Dk. Mwakibinga.

Amesema watanzania wanahitaji kitu bora, hivyo serikali nayo inawaandalia sheria na kanuni bora ambazo zitatumika katika rufani za manunuzi.

Hata hivyo amesema pamoja na kufanya maboresho baada ya kupokea maoni, pia kutakuwa na nafasi ya wadau mbalimbali kutoa maoni yao kwa njia ya mtandao ili nayo yafanyiwe kazi.

Related Posts