Sunzu, Maftah watia neno Derby

MASTAA wa zamani wa Simba na Yanga, Felix Sunzu na Amir Maftah wametofautiana mitazamo kuhusu mchezo wa dabi ya Kariakoo utakaochezwa Jumamosi ya Aprili 20 kuanzia saa 11 jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, ambao mzunguko wa kwanza Yanga ilishinda kwa mabao 5-1.

Sunzu raia wa Zambia aliyekuwa mmoja ya wafungaji wakati Yanga ikifungwa mabao 5-0 na Simba katika dabi iliyopigwa Mei 6, 2012 na aliyeamua kuweka maskani yake hapa nchini, amesema haiwezekani Yanga ikaifunga Simba nje ndani, huku akiwataka mashabiki wa mnyama kutoingiwa unyonge.

“Dabi ni dabi. Sikatai, Yanga wapo vizuri na wanacheza mpira mzuri, lakini mchezo huu hauangalii nani yuko vizuri, mchezo utabadilika, hivyo mashabiki wasilete shida na kukata tamaa mapema,” amesema Sunzu aliyewahi kukipigana Al Hilal ya Sudan na klabu kadhaa za Zambia aliyeongeza;

“Mashabiki wasitie uoga, watoe hofu ile ni dabi, Simba inaweza kushinda 1-0 ama ikaisha kwa sare. Yanga haiwezi kuifunga Simba mara ya pili, najua mpira wa Tanzania Simba na Yanga hii haiwezekani kwa hiyo wasiwe na hofu wawe na matumaini kwa Simba.”

Kwa upande wa nyota wa zamani wa timu hizo, Amir Maftah alisema Yanga inakwenda katika mchezo huo ikiwa na mwendelezo mzuri wa matokeo na hesabu zikiibeba, lakini akaonya Wana Jangwani hawapaswi kubweteka.

“Simba ijipange vizuri kwa sababu mtani wao yuko vizuri katika kila nyanja, wapunguze makosa kwenye ulinzi, ndilo eneo ambalo mimi naliona lina tatizo, pia watu wa mbele waje kuwasapoti mabeki,” alisema Maftah na kuongeza;

“Wenzao Yanga mpira ukipotea wanaanza kukaba mara moja, lakini Simba wanatoa mianya anaposhambuliwa, hivyo wajitahadhari na hilo, lakini Yanga wasijikweze sana kwa sababu mpira ni dakika 90.”

Simba na Yanga zinakutana kila moja ikitoka kupata matokeo tofauti katika mechi zilizopita za Ligi Kuu na Wekundu ilitoka  sare ya 1-1 na Ihefu ugenini mjini Singida, wakati watani wao wakishinda mabao 2-0 dhidi ya Singida FG pia ikiwa ugenini jijini Mwanza.

Kwa sasa Yanga ipo kileleni mwa msimamo ikiwa na pointi 52 kutokana na mechi 21 ikifunga mabao 52 na kufungwa 11 tu, ilihali Simba ikiwa ya tatu na alama 46 baada ya mechi 20, imefunga mabao 40 na kufungwa 19 na Azam FC ni ya pili ikiwa na pointi 51 baada ya mechi 23 baada ya jana usiku kulazimishwa suluhu na Mashujaa.nzu

Related Posts