Benki ya NMB imekabidhi pikipiki 20 zenye thamani ya zaidi ya Sh 65 milioni zitakazosaidia kuimarisha ulinzi mkoani Arusha. Anaripoti Mwandishi Wetu, Arusha…(endelea).
Mchango huo ambao umetolewa kwa Jeshi la Polisi mkoani humo unaendana na mpango mkakati wa benki hiyo wa kuendeleza sekta ya utalii unaolenga kuimarisha mifumo endelevu ya ikolojia ya utalii.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya pikipiki hizo ambayo ilihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda iliyofanyika katika Tawi la NMB Clock Tower jijini Arusha leo Jumatano, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa benki ya NMB, Filbert Mponzi amesisitiza dhamira ya benki hiyo kuendelea kufanya kazi kwa karibu na wadau wote ikiwemo Serikali kusaidia maendeleo ya sekta ya utalii.
“Kwetu mkoa wa Arusha ni muhimu na ni wakimkakati kwa kuwa ni kitovu cha watalii ndomana leo tupo mahali hapa kukabidhi pikipiki 20 ili kuimarisha usalama. Kama benki, tunaamini kwamba usalama ukiimarishwa, sekta ya utalii itastawi kwa kiwango kikubwa,” amesema.
Mponzi ameonyesha matumaini kuwa juhudi za benki hiyo mkoani Arusha zitakuwa na athari kubwa zaidi katika mnyororo wa thamani wa sekta ya utalii nchini kote.
“Juhudi zetu zitakuwa chachu ya ukuaji wa sekta ya utalii kwa ujumla. Tunaamini kuwa watalii wakiwa salama hapa Arusha kama kitovu cha utalii, basi watakuwa tayari kwenda kufurahia maeneo utali katika maeneo mengine nchini kama vile Zanzibar, amesisitiza.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Waongoza Watalii Wazawa nchini, Samuel Diah wakati wa hafla hiyo aliipongeza Benki ya NMB kwa mchango huo akionyesha imani kuwa kwa kiasi kikubwa utachochea ukuaji wa sekta ya utalii mkoani humo.
“Kwa kweli mchango huu umekuja wakati muafaka kwani kuhakikisha usalama wa watalii wa ndani na nje ni kipaumbele kikuu kwetu kwa sasa. Juhudi za Benki ya NMB zitahakikisha usalama wa mkoa wa Arusha wakati wote na vile utachangia juhudi za Serikali ya awamu ya sita za kukuza sekta ya utalii,” amesema Diah.
Ameongeza, “Usalama ndio kivutio kikubwa kwa watalii wote. Pamoja na mkoa wa Arusha kuwa na vivutio vingi vya utalii, hatuwezi kuvutia watalii wengi kama mkoa hauko salama,”
Dia ametumia hafla hiyo kumpongeza Mkuu wa Mkoa wa Arusha kwa kuanzisha kampeni ya kuliwezesha jeshi la polisi kwa kutumia pikipiki, huku akisisitiza kuwa mpango huo hatimaye utaongeza ufanisi wa jeshi hilo katika utoaji wa huduma.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda wakati wa hafla hiyo amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa mstari wa mbele katika kutangaza vivutio vya kipekee vya Tanzania na kuwataka wananchi kulinda vivutio hivyo vya utalii.
“Hili ni tukio la kihistoria na hakika ni ishara ya kurudisha kwa jamii. Wananchi wanatakiwa kusaidia makampuni yanayowajibika kama Benki ya NMB,” amesema.
Makonda aliongeza, “Pikipiki ambazo zimetolewa leo hazitasaidia jeshi la polisi bali jamii nzima ya mkoa wa Arusha kwani zitasaidia kuimarisha ulinzi na kuhakikisha usalama wa raia na mali zao.
Katika hafla hiyo, alitoa wito kwa wakazi wote wa mkoa wa Arusha kuendela kushirikiana kwa karibu na jeshi la polisi kwa kuwabaini wahalifu wote mkoani humo.