Dar es Salaam. Wadau wa ujuzi wa kidijitali, wameiomba Serikali kutengeneza sera itakayowasaidia wabunifu na wavumbuzi kushiriki katika masuala ya teknolojia kwa sababu kuna vijana wana mawazo ya kibunifu lakini sera zilizopo zinawasababisha kushindwa kufanya kazi kwa ukamilifu.
Hayo yamesemwa leo Jumatano Mei 22, 2024 na mwezeshaji kutoka Kitengo cha Ubunifu cha Youth 4 Children Innovation Hub, kinachopatikana katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Millenium Anthony, katika mdahalo wa majadiliano uliokuwa ukijadili Ujuzi wa Kidijitali kwa Maendeleo ya Rasilimaliwatu katika wiki ya ubunifu kwa mwaka 2024, yenye kauli mbiu, “ubunifu kwa uchumi shindani.”
Wiki ya ubunifu imeandaliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech) na Mradi wa Ubunifu wa Funguo chini ya Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa(UNDP).
Anthony amesema licha ya vijana kuwa na mawazo mazuri ya ubunifu, wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo upatikanaji wa vifaa, mfano kompyuta, fedha, intaneti na hivyo kukosa nafasi ya kufanya vizuri katika bunifu zao.
“Ni vizuri Serikali ikasikiliza changamoto za vijana na kuzifanyia kazi, niwaombe Serikali iwekeze vijana katika masuala ya teknolojia na intaneti ili vijana,” amesema Anthony ambaye kupitia safari yake ya kidijitali, aliona nguvu ya mabadiliko ya teknolojia na uvumbuzi.
Meneja Programu wa Funguo chini ya UNDP, Joseph Manirakiza amesema ni muhimu watunga sera na wadau wengine wa maendeleo kuwezesha na kusaidia wabunifu wanaoanza ubunifu na wavumbuzi ili wafanikie malengo yao badala ya kuweka kanuni kali na zenye vikwazo.
Amesema ni vizuri watunga sera wakajiunga mijadala kuhusu masuala ya kidijitali ili kusikiliza changamoto mbalimbali wanazokutana nazo wabunifu na wavumbuzi na kuzichukua na kuzifanyia kazi.
Amesisitiza kuwa mwelekeo uliopo sasa ni kusaidia wanaoanza ubunifu na wavumbuzi badala ya kuweka kanuni kali na kwamba kuwepo kwa mbinu hiyo, itakuza uvumbuzi na kukuza ukuaji wa uchumi kidijitali.
“Kuna mengi yanayotokea katika maeneo ya kidijitali yanayohitaji majadiliano, kwa kuwa sote bado tunajifunza na kuzoea hili, ni muhimu kufahamu jinsi ya kuwashirikisha na kuwapa ujuzi watunga sera ofisini ili kuunda na kutekeleza sera husika ya kidijitali,” amesema Manirakiza
“Kama washikadau na vile vile watunga sera tuzingatie kuwezesha na kusaidia waanzishaji na wavumbuzi. Tunapaswa kutanguliza kuwasaidia wafanikiwe badala ya kuzingatia kuweka kanuni zenye vikwazo,”
Mkuu wa Idara ya Elimu kutoka Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (Unicef) Dk Daniel Baheta amesema katika mazingira ya kisasa ya kiteknolojia yanayoendelea kwa kasi, vijana hawawakilishi tu kizazi kijacho bali pia nguvu ya mabadiliko waliyoipata kwa kizazi kilichopita.
Amesema ni muhimu kwa vijana kuhama kutoka kuwa watumiaji wa kawaida hadi kuwa wabunifu wa teknolojia, wakijumuisha jukumu la waleta mabadiliko katika jamii.
“Vijana ni kizazi kijacho na nguvu ya kubadilisha wakati wetu. Ni muhimu kwao kubadilika kutoka kuwa watumiaji tu wa teknolojia hadi kuwa wabunifu wa teknolojia na kuwa waleta mabadiliko” amesema Dk Baheta.
Kwa upande wake, wakili Chacha Mwita kutoka Taasisi ya Juction of Hope Foundation, amesema wiki ya ubunifu inawaleta pamoja wabunifu na kubadilishana uzoefu.
“Mimi nimekuja kwa ajili ya kupata uzoefu na kujifunza kutoka kwa wenzetu waliofanikiwa,” amesema Mwita.