Dar es Salaam. Wakati wadau wa sekta ya mawasiliano wakisema ili tatizo la kukosekana kwa intaneti lisijirudie kunapaswa kuongezeka kwa wawekezaji wanaotoa huduma hiyo, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema Serikali imewasikia na inaendelea na mchakato wa kuwa na satellite yake.
Haya yanajiri ikiwa zimepita takribani siku kumi tangu lilipotokea tatizo la intaneti lililodumu kwa takribani siku mbili kuanzia Mei 12, 2024 na kusababisha adha kubwa kwa watumiaji wa huduma hiyo.
Kukosekana kwa intaneti ilitokana na huduma za nyaya za baharini kama Seacom na EASSy kupata hitilafu kwenye nyaya hizo zilizoko kati ya Msumbiji na Afrika Kusini.
Kutokana na kadhia hiyo, Kampuni ya Mwananchi Comunications Limited (MCL) leo Jumatano, Mei 22, 2024 imeandaa mjadala wa X-Space ukiwa na mada: “Tufanye nini tatizo la kukosekana kwa Intaneti lisijirudie.”
Mjadala huo uliodumu kwa dakika 120 kuanzia saa 2:00- 4:08 usiku, umeshirikisha wadau mbalimbali wa mawasiliano waliochangia kwa mitazamo tofauti akiwamo Waziri Nape na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Mhandisi Peter Ulanga.
Wadau waliochangia wamesema lazima kama nchi iwe na wataalamu wa kutosha wa masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) na utolewaji wa elimu kwa wananchi unapaswa kuongezwa.
Mwendeshaji ‘Sikio podcast’, Belinda Lifard amesema, “tunapaswa kujiandaa na changamoto za mtandao zisizojulikana.”
“Tatizo hili la mawasiliano ni changamoto na fursa, Tanzania tunapaswa kujiandaa na changamoto zisizojulikana, hakuna aliyewahi kuwaza tutapata shida ya mtandao, hivyo tunaweza kujiandaa kwa miaka ijayo. Maendeleo yanavyozidi kukua ndipo matumizi ya mtandao yanavyoongenezeka hivyo tunapaswa kujipanga kwa changamoto zisizojulikana,” amesema Belinda.
“Pia, kiuchumi ni fursa inaweza kutumika kuwezesha wataalamu wetu wanaohusika kwenye maeneo yote kwenye eneo hili na Serikali iwe na miundombinu ya kuwezesha kurejesha mawasiliano ndani ya muda mfupi yanapokatika.”
Naye Stanley Kabula akichangia mjadala huo amesema kitu cha kufanya, tumeshaona madhara kwa shughuli kutofanyika, kijamii kuna haja ya nchi nyingi za Afrika kutoa elimu kwa jamii.
Kabula amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau ihakikishe inawaongeza wenye utaalamu kwenye masuala ya Tehama.
“Hatuwezi kurejesha mawasiliano kama hatuna wataalamu wa mawasiliano wenye uwezo wa kusimamia.
“Hii inaleta heshima na usalama wetu wa ndani, ikiwezekana Serikali itenge bajeti kila mwaka kuwe na wataalamu angalau 50 wanaokwenda kusomea masuala ya Tehama,” amesema.
“Elimu inapaswa kutolewa, tusidharau tu kwamba Dar es Salaam ndio watumiaji wakubwa wa intaneti, Serikali ina haja ya kutoa elimu kuanzia shuleni kuhusu matumizi ya teknojia, faida na hasara zake hii itakuwa na faida chanya, tumeona upotoshaji mkubwa ulivyosambaa mtandaoni baada ya mtandao kukatika.
“Kusambaa kwa taarifa potofu kunachangia uwepo wa taharuki kwenye jamii, kiuchumi, Serikali itenge miundombinu rafiki kuleta huduma ya intaneti kwa karibu,” amesisitiza. “Tunatamani kampuni za nje zije kuwekeza hapa nchini, kwa nini zinashindwa hatuwezi kuziruhusu kampuni za kigeni kuja wakati tuna changamoto ya kimsingi hasa miundombinu haijakaa sawa.”
Mchangiaji mwingine Geofrey Geofrey amelia na gharama za vifurushi vya intaneti akisema zimepanda ukilinganisha na hapo awali.
“Mtandao ni suala endelevu linaloisaidia nchi kufika, ukiangalia mabando yanayouzwa ni kuanzia Mbs 200, Mbs zimepanda, gharama za maisha zimepanda na vocha zimepanda.
“Kwa hiyo ninachoomba Bunge likae lifanyie marekebisho masuala ya mtandao na kubandilisha kwa vifurushi, sisi watumishi wa chini tunashindwa kutekeleza majukumu yetu kwa wakati kutokana na gharama za mtandao kuwa juu,” amesema.
Awali, akichokoza mada hiyo Mhariri wa Uchumi wa Gazeti la Mwananchi, Ephrahim Bahemu amesema tatizo la kukosekana kwa intaneti lilitokana mkongo wa baharini kukatika, ukiangalia mikongo ya baharini inayounganisha Tanzania na ulimwengu zipo mbili, kilichotokea sisi tunatumia mkongo wa kusini ambao ulipata hitilifu.
Amesema suluhu ni kuwa na watoa huduma wengi, kadiri tunavyokuwa na watoa huduma ili ikitokea shida tutaendelea kuunganishwa na ulimwengu.
“Kuna haja ya kuendelea kuvutia wawekezaji hasa ukiangalia maisha yetu yapo kwenye dijitali, na uwekezaji wa mkongo wa Taifa hauepukiki. Pia, tuwe na viunganisho mbadala (link) ili tatizo linapotokea tuwe na njia mbadala,” amesema Bahemu.
Baada ya michango hiyo, Waziri Nape ameanza kwa kuipongeza Mwananchi kwa kuandaa mjadala huo akisema Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeanzisha klabu za kidijitali za masuala ya Tehama shuleni.
Pia amesema, Serikali imesikia wachangiaji wengi wakikiri tunauelewa mdogo wa masuala ya mawasiliano na changamoto, hii inaweza kusababisha taharuki: “Hivyo nimepokea ushauri wa Serikali kuendelea kutoa elimu.”
“Serikali tunajenga chuo kikubwa Dodoma kwa kushirikiana na Wakorea na nyingine Kigoma halafu tutakuwa na vituo atamizi nane kwa ajili ya kufundishia masuala haya ya Tehama,” amesema Nape.
Amesema hayo ni baadhi ya mambo yanayoongeza uelewa wa haya mambo jinsi yanavyoenda.
“Inawezekana tunaonekana tukilinganishwa na majirani zetu hatujapiga hatua kubwa lakini tumepiga hatua kubwa kuliko wenzetu na wao wamepiga kuliko sisi.
“Katika Bara la Afrika kuna tathmini ya usalama mtandaoni huwa inafanyika Tanzania ni nchi ya pili kwa usalama wa mtandao Afrika, inawezekana hatua tunazopiga zingine tupo nyuma, lakini wizara inayoshughulikia Tehama imeanzishwa mwaka 2021.”
“Sasa ni vizuri kujua miaka ya nyuma tulikuwa tunatumia satellite kabla ya mkongo, mpaka 2008 hadi 2009 baada ya dunia kuona upungufu kwenye satellite wakaamua kuja na mfumo wa kebo, mfumo huu ulipoanzishwa ukafanyika uamuzi Serikali kukoa fedha kujenga mkongo wetu wa ndani na kuanzia kupokea kebo za baharini.
“Kwa hiyo mwaka 2009 ndio tukaanza kupata huduma ya mkongo hivyo tuna uzoefu wa satellite. Ukweli ni kwamba huduma za kebo ni bora kuliko satellite, ni bora, zina kasi na ni salama hivyo satellite ni njia mbadala tu za kutoa huduma,” amesema.
Waziri Nape amesema Serikali inaona umuhimu wa kuwa na satellite yetu na tupo hatua nzuri na suala la ununuzi wa satelite ya nchi si kama kununua nyanya ni mchakato wa muda mrefu.
“Tulianzisha hili kwenye bajeti iliyopita, tumeanzisha kamati, tupo hatua za mbele sana kufikia kuwa na satelite yetu,” amesema Nape.
Katika maelezo yake, Waziri Nape amesema: “Hata nchi zilizoathirika na intaneti zilikuwa na satellite, ndio maana nasema satellite inategemea hali ya hewa ina changamoto nyingi sana ambazo nasema si njia nzuri ya kuwasiliana ndio maana dunia iliweka kebo kuwasiliana.”
“Hii huduma tunayotumia ni huduma mbadala, kuna mtu anasema tuwe na kebo yetu wenyewe niseme kuwa hakuna gharama ya kupitisha kebo baharini na usalama wake lazima iwe ni mshikamano wa nchi,” amesema Nape.
Waziri huyo amesema kwa jiogorafia tuliyonayo tutaongeza idadi ya kebo ili inapokatika moja tuunganishe nyingine.
“Kama Serikali hatuwezi kusema tatizo hili haliwezi kutokea tena, unajua janga lolote linaweza kutokea ikaleta shida, jambo la msingi ikitokea tunaondoka vipi kurejesha huduma kwa muda mfupi madhara yasiye makubwa,” amesema.
Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Mhandisi Peter Ulanga ni miongoni mwa washiriki wa mjadala huo ambaye amegusia tatizo hilo akisema kwanza halikuanza wiki iliyopita bali tangu Januari 2024.
“Tunapopima matumizi ya teknolojia gani itumike mfano satellite au mkongo, satellite ni ghali zaidi ukienda kwenye ukurasa wa starlink, ili kutengeenza ‘community hub’ itakugharimu Dola milioni 1.2 za Marekani na utalipia kwa mwezi gigabits moja Dola 75,000 ambayo ni tofauti na kebo,” amesema Mhandisi Ulanga akielezea njia mbadala ya huduma hizo.
Aidha amesema wameboresha miundombinu na ikitokea tatizo kama hilo waweze kurejesha huduma.
“Kuna kebo zinajengwa kutoka Kigoma kwenda nchini DR Congo ili ikitokea upande wa mashariki basi zitumike za upande wa magharibi,” amesema.