Chongolo aja na mbinu mpya ujenzi vyoo bora kwa kaya

Songwe. Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo amesema anaanzisha mashindano ya ujenzi wa choo bora wilayani Momba na kaya itakayoibuka na ushindi itajipatia mifuko mitatu ya mbolea.

Hatua hiyo imekuja zikiwa zimepita siku chache tangu Mganga Mkuu wa Mkoa huo, Dk Boniface Kasululu kufanya ukaguzi wa vyoo katika kijiji cha Mkutano wilayani Momba na kubaini kati ya kaya 320, kaya 128 hazina vyoo huku wananchi wakijisaidia kwa kuchimba mashimo nyakati za usiku.

Akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Namin’gon’go leo Jumatano Mei 22, 2024, Chongolo amesema ili kuhamasisha kila kaya iwe na choo bora, ataanzisha mashindano na washindi watapatiwa mifuko ya mbolea.

Amesema Septemba na Oktoba, mwaka huu atapita kufanya ukaguzi maalumu wa ujenzi wa vyoo bora ndipo atakapozipata kaya zitakazoibuka na ushindi.

Amesema kaya itakayoibuka na ushindi wa kwanza ataipatia zawadi ya mifuko mitatu ya mbolea mshidi wa pili atajibebea mifuko miwili na mshindi wa tatu atajinyakulia mfuko mmoja.

“Nimefika kwenye kaya moja nimeshangaa ukuta wa choo unanifika kwenye kiuno, sasa nikajiuliza hawa watu vipi, lazima hili suala tulibebe kama ajenda ya mkoa mzima kunusuru magonjwa ya mlipuko,” amesema Chongolo.

Aidha, amewataka wadau wa mazingira mkoani Songwe kuweka mikakati itakayowasaidia wananchi kubadilisha mtazamo juu ya ujenzi wa vyoo bora na usafi wa mazingira.

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Boniface Kasululu amesema hivi karibuni aliongoza timu kutoka mkoani iliyokuwa ikihamasisha ujenzi wa vyoo bora katika Kijiji cha Mkutano na wakabaini kaya ambazo hazina vyoo bora wananchi huchimba shimo dogo kando ya nyumba na kujisaidia haja kubwa kisha kulifukia.

Amesema hali hiyo inahatarisha usalama wa afya za watu hao na ameomba wananchi kushirikiana na serikali kuitikia wito kujenga  vyoo bora.

Akizungumzia hilo, Mchungaji wa Kanisa la Neema, Nestori Matofali amesema hali ni mbaya, wananchi wengi wanajisaidia hovyo hali inaashiria mlipuko wa magonjwa ya kuambukiza kikiwamo kipindupindu  na ya tumbo.

“Kama mkuu wa mkoa atafanikiwa kuanzisha mashindano na kutoa zawadi ya mifuko ya mbolea kwa wananchi watakaojenga vyoo hivyo itakuwa hamasa nzuri labda wataepukana na tabia hii ya kujisaidia vichakani,” amesema Mchungaji Matofali.

Naye Mariamu Sichalwe mkazi wa Kijiji cha Mkutano, amesema kukosekana kwa vyoo bora kijijini hapo kunatokana na viongozi kutowapatia elimu ya ujenzi wa vyoo bora.

“Bado wananchi wa huku wanaishi yale maisha ya kale, sasa hii ni mbaya wanapaswa kubadilika,” amesema.

Related Posts