Mamia ya wadau wa riadha nchini wamejitokeza katika mazishi ya aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha riadha mkoa wa Pwani, Joseph Luhende.
Luhende ambaye amewahi kuwa kocha wa klabu mbalimbali alifikwa na mauti Jumamosi iliyopita na kuzikwa jana Mei 21 nyumbani kwake Kibaha mkoani Pwani.
Miongoni mwa wadau hao ni nyota na bingwa wa zamani wa Afrika wa marathoni, Juma Ikangaa na bingwa wa zamani wa dunia wa nusu marathoni, Filbert Bayi.
Kwa nyakati tofauti nyota hao walimzungumzia Luhende kama miongoni mwa wadau wa mchezo huo nchini.
Hadi mauti inamkuta, Luhende alikuwa ni Mwenyekiti wa Chama cha Riadha mkoa wa Pwani na mjumbe wa mkutano mkuu wa Shirikisho la Riadha (RT).
Naibu Katibu mkuu wa Chama cha Riadha mkoa wa Pwani  Elias Hotay amesema wamempoteza kiongozi mahiri aliyekuwa na mchango katika riadha kwenye mkoa huo.
Hotay amewashukuru wadau wote walioguswa na msiba huo na kushirikiana na familia katika mazishi ya kiongozi huyo.