Dar es Salaam. Wakati mchango wa sekta ya mifugo katika Pato la Taifa ukishuka kutoka asilimia saba mwaka 2021 hadi asilimia 6.7 mwaka 2022, Kampuni ya Bima ya CRDB na ACRE Africa zimesaini Mkataba wa Makubaliano (MoU) kwa ajili ya kuikuza sekta hiyo.
Takwimu za kushuka kwa mchango wa sekta hiyo, zimetolewa katika hotuba za bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi za mwaka 2024/25 na ile ya 2023/24.
Akizungumza wakati wa utiaji saini makubaliano hayo leo Jumatano Mei 22, 2024 Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bima ya CRDB, Wilson Mnzava amesema lengo ni kuboresha hali ya usalama wa chakula, hususani miongoni mwa wafugaji kwa kutoa suluhu ya changamoto hizo.
“Moja ya changamoto kubwa inayolikabili Bara la Afrika leo ni usalama wa chakula, vitisho vinavyotokana na mabadiliko ya tabianchi vinaendelea kukwamisha uzalishaji wa chakula, hivyo kuhatarisha maisha ya mamilioni ya wakulima na wafugaji,” amesema.
“Kampuni ya Bima ya CRDB, tunatambua uharaka wa upatikanaji wa chakula. Changamoto hizi na tumejitolea kutoa suluhu ambazo zitawasaidia wakulima na wanyama wao katika kukabiliana na hali hizi zisizo na uhakika,” amesema Mnzava.
Makubaliano yamesainiwa ikiwa ni miongoni mwa utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Serikali wa Kukuza Sekta ya Fedha 2020-2030 unaozitaka kampuni za bima kubuni bidhaa zinazoendana na mahitaji ya watu.
“Kampuni za bima zinahimizwa kubuni bima zinazotoa suluhu katika mahitaji ya watu,” imesema sehemu ya mpango huo.
Kuhusu namna ya kufikia wakulima hasa wafugaji waliolengwa na bima hiyo, Mnzava amesema: “Kwa kutumia mtandao wetu mpana wa matawi na wakala wa Benki ya CRDB, tunaweza kufanya huduma hizi muhimu za bima kuwafikia wananchi wetu. Dhamira yetu ni kuhakikisha wakulima kote nchini wanapata msaada wanaohitaji ili kulinda maisha yao na kuchangia usalama wa chakula wa Taifa.”
Mtaalamu wa Uchumi, Mack Patrick akizungumzia mchango wa bima katika sekta ya kilimo amesema utaleta ahueni katika uchumi na maisha ya jamii za wafugaji.
“Kuna jamii zinafanya shughuli muhimu kwa uchumi wa nchi lakini hazifikiwi na huduma mbalimbali, wakiwamo wafugaji na muda mwingine hata wakulima. Kuwapo kwa bima hii kutawapa kinga wafugaji katika shughuli zao na mali wanazomiliki ikiwamo mifugo,” amesema.