DILI la Yanga na beki Chadrack Boka wa FC Lupopo limeingia ugumu baada ya pande zote mbili kukaa mezani kwa saa saba bila kufikia muafaka.
Mwanaspoti limejiridhisha kwamba bosi wa nyota huyo, Jacques Kyabula Katwe alitua Dar es wikiendi iliyopita kwa ndege binafsi pamoja na ishu zake binafsi, lakini pia alikuja kukamilisha dili hilo. Lakini kasheshe imekuja kwenye mkwanja.
Mabosi hao walikutana mara mbili juzi usiku kwa saa tatu na jana asubuhi walikaa saa nne bila kufikia muafaka wowote, huku kila mmoja akiweka dau lake mezani.
Wakongomani hao wanataka Dola 110,000 (zaidi ya Sh285 milioni) ili waweze kumuachia beki huyo wa kushoto mwenye mkataba wa mwaka mmoja na FC Lupopo na mmoja wa watu waliopo kwenye msafara wa tajiri huyo wanadai ni dau la kawaida kwa wachezaji wao, ingawa Yanga kikaoni waliwaambia kwamba washuke kidogo.
Lakini, vigogo hao waligoma wakawaambia wapo tayari kutoa Sh230 milioni. Mwanaspoti linajua kwamba wamepeana siku tano kuanzia jana za kutafakari juu ya ofa ya kila mmoja ili kuweka wepesi kwa pande zote mbili kufikia muafaka.
Baada ya mazungumzo hayo FC Lupopo iliweka wazi kwamba thamani ya mchezaji huyo ni ya kawaida hasa ukizingatia kwamba ana uwezo wa kucheza kushoto na ni tishio kwenye kutengeneza nafasi na mipira ya krosi.
Mwanaspoti linajua kwamba viongozi hao wa staa huyo wameondoka jana kurejea DR Congo na wanasubiri simu ya Yanga.
Kama dili hilo litakamilika, basi beki huyo atakwenda kuwa mrithi wa Mkongomani mwenzake, Joyce Lomalisa anayemaliza mkataba wake na Yanga mwisho wa msimu huu, huku akiwa hana kiwango bora kutokana na majeraha ya mara kwa mara yaliyomfanya kushindwa kucheza baadhi ya mechi muhimu.
Hilo linamfanya Boka kuwa na nafasi ndani ya kikosi hicho, licha ya kuwa atakwenda kucheza nafasi moja na mzawa Nickson Kibabage mwenye bao moja na asisti nne.
Yanga imepania kumaliza dili zote kubwa mapema kabla ya msimu kumalizika ili kila mmoja ajue hatima yake mapema kabla ya msimu wa maandalizi kuanza.
Mwanaspoti linajua kwamba yatafanyia mabadiliko kadhaa haswa kwa wachezaji wageni ili kuboresha zaidi kikosi na kuingia na nguvu kubwa kwenye msimu wa Ligi ya Mabingwa Afrika.