SIMBA imeshtuka hii ni baada ya kuamua kumuita kiungo mkabaji, Mzamiru Yassin haraka kwa ajili ya makubaliano ya mkataba mpya baada ya baadhi ya timu kuonyesha nia ya kumhitaji.
Kiungo huyo ambaye amehudumu kwa muda mrefu ndani ya kikosi cha Simba alikuwa anawindwa na Azam FC sambamba na Ihefu FC, timu ambazo zilikuwa zinataka huduma ya mchezaji huyo msimu ujao.
Staa huyo ambaye amemudu kupata nafasi ya kucheza chini ya makocha mbalimbali waliopita ndani ya timu hiyo, ataendelea kusalia Msimbazi hadi 2027 kwa dau la zaidi ya Sh200 milioni, ingawa inaelezwa kuna makubaliano mengine ambayo yataendana na utendaji.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba kimeliambia Mwanaspoti kuwa mazungumzo kati ya pande zote mbili yamekwenda vizuri na kiungo huyo atasaini mkataba mapema wiki ijayo.
Mmoja wa vigogo wa Simba alisema wanaendelea na usajili kimyakimya na watabakiza wachezaji wote ambao wanaamini wataipambania timu hiyo msimu ujao ingawa watapukutisha majina makubwa.
Kiungo huyo wa Simba ameweza kupambana na mastaa wengi wa kigeni waliopita hapo akiweno Sadio Kanoute na Fabrice Ngoma ambao licha ya ubora walionao amefanikiwa kupata namba mbele yao.
Mzamiru aliyejiunga na Simba, Juni 2016, akitokea Mtibwa Sugar anaungana na beki Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ kuwa kwenye rekodi ya wachezaji waliocheza ndani ya timu hiyo kwa muda mrefu.
Siyo tu Mzamiru, hivi karibuni Simba ilizima jaribio la straika mzawa, Kibu Denis ambaye alikuwa amefikia pazuri na Yanga, na ilishampa mpaka nakala ya mkataba aliokuwa anatembea nao ambao ulikuwa na thamani ya zaidi ya Sh250 milioni ambazo na Msimbazi wamefinyanga na kumpanga mchezaji akalainika.
Usajili wa timu mbalimbali nchini umeanza baada ya msimu kubakisha mechi mbili kukamilika, huku Yanga ikiwa tayari bingwa wa Ligi Kuu Bara wakati Simba na Azam zikiwania nafasi ya pili.