Dar es Salaam. Wakati Serikali ikianza utekelezaji wa kuweka mita za malipo ya huduma za maji kwa kadiri mtu anavyotumia (Luku), Shirika la WaterAid limeanza kutekelezaji kwa kuwafungia wananchi mita hizo.
Akiwasilisha bajeti ya Wizara ya Maji 2024/25 bungeni Dodoma Mei 9, 2024, Waziri Jumaa Aweso alisema kuwa matumizi ya mita za maji za malipo ya kabla zitaongeza ufanisi wa matumizi ya maji pamoja na kudhibiti kuvuja maji kunakosababisha hasara kwa mteja.
Alisema kupitia Mamlaka za Maji na Jumuiya za Watumiaji wa Maji (CBWSOs) zimeendelea kuwafungia wateja ambapo hadi Aprili 2024, wateja 13,526 walikwishapata huduma hiyo katika mikoa ya Dodoma, Iringa na Tanga.
Akizungumza jana Mei 21, 2024 kuhusu uwekaji wa mita hizo, Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la WaterAid Tanzania, Anna Tenga Mzinga amesema mwaka 2018, waliingia ubia na kampuni ya EwaterPay na kufunga mita za malipo ya awali katika Kijiji cha Sangara kilichopo Mkoa wa Manyara.
Amesema katika kijiji hicho wamewafikia watu 2,000 na kisha mwaka 2021 kupitia mradi wa maji wa vijiji vitano wilaya ya Arumeru mkoa wa Arusha kufunga mita za maji za malipo ya kabla na kufikia takribani wananchi 23,000.
“Kupitia miradi hii miwili, mwananchi alikua na uwezo wa kujaza pesa katika simu yake ili kulipia tokeni maalumu inayotumika kuchotea maji na kwa kiasi cha shilingi 30 kupata ndoo moja ya maji ya lita 20, fedha ambayo huingia moja kwa moja kwa kikundi cha watumia maji (CBWSO),” amesema.
Amesema miradi mingine iliyotekelezwa kwa kuiga ubunifu huo ni pamoja na mradi wa bwawa la maji Kwamaizi, na Itigi, Singida.
“Tunaipongeza Serikali kwa kuasili mfumo huu, sisi tunaamini sana katika ubunifu na ni moja ya nyenzo muhimu tunayotumia katika kutekeleza na kuwasilisha miradi yetu.
“Tutaendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika kubuni miradi mipya inayotumia teknolojia na kuifanyia tathmini zitakayorahisisha kujifunza na hatimaye kuleta matokeo chanya ya upatikanaji wa maji hasa katika kumtua mama ndoo kichwani nchini Tanzania” amesema.
Amesema shirika hilo limejipanga kujikita kimkakati katika Wilaya ya Hanang, Mkoani Manyara katika kipindi cha utekelezaji wa mpango mkakati.
“Utekelezaji katika wilaya hii utasaidia kuonesha mifano hai ya utekelezaji, ubunifu na ushirikishwaji ambayo inaweza kusaidia kumfikia kila mwananchi na huduma endelevu na salama za maji, usafi wa mazingira na usafi binafsi ambayo inaweza kuigwa na kutekelezwa katika maeneo mengine.