Watu 11 wamefariki dunia na wengine wawili kujeruhiwa baada ya mfumo wa joto wa kiwanda cha kuzalisha sukari cha Mtibwa Sugar kulipuka wakati wakijiandaa kuanza uzalishaji wa sukari kwenye kiwanda hicho kilichopo Turiani mkoani Morogoro.
Akizungumza na Mwananchi digital leo Alhamisi Mei 23, 2024 Kamanda wa Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro, Shaban Marugujo amesema mlipuko huo ulitokea saa 7 usiku na umeua 11 na wengine wawili kujeruhiwa.
“Ni kweli watu 11 wamefariki dunia na wengine wawili kujeruhiwa baada ya mlipuko wa mpira wa joto wakati wanajiandaa na uzalishaji wa sukari pale kiwandani, ifahamike kwamba ili sukari ichakatwe kuna kiwango cha joto ambacho kinatakiwa kifikie sasa wakati maandalizi ya uzalishaji yakifanyika na kile kiwango cha joto kikingojewa ndipo ukatokea mlipuko huo na kuwakuta watu hao 11 ambao kwa kiwango kile cha joto wakafariki papo hapo,”
“Chanzo halisi cha mlipuko huo bado hatujakipata ila bado tunaendelea na uchunguzi, timu nzima iko hapa kiwandani tangu usiku huo na mpaka sasa tunaendelea na tukikamilisha tutatoa taarifa rasmi” amesema Marugujo.