BATO ya ufungaji wa mabao ya Ligi Kuu Bara, baina ya viungo Stephane Aziz Ki wa Yanga na Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam FC, inaweza ikajirudia ilivyokuwa katika msimu wa 2021/22 kati ya George Mpole na Fiston Mayele anayeichezea Pyramids ya Misri kwa sasa.
Katika msimu wa 2021/22, Mayele akiwa Yanga na Mpole alikuwa Geita Gold ulitokea ushindani baina yao ambapo mechi za mwisho ndizo zilizoamua nani achukue kiatu cha dhahabu.
Mpole ndiye aliyechukua tuzo ya ufungaji bora akimaliza na mabao 17, ilhali Mayele alimaliza na 16 ingawa msimu uliofuatia wa 2022/23 Mkongomani huyo alifikia mabao 17aliyogongana na Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’ wa Simba, hivyo wote wawili wakapata kiatu cha dhahabu.
Kinachoendelea kwa Fei Toto kufikisha mabao 16 na Azi Ki mabao 15 (kabla ya meche ya jana), kimemuibua Mpole anayeichezea FC Lupopo ya DR Congo kueleza namna wachezaji hao wanavyokuwa kwenye presha na kunogesha ligi.
“Nimependa uwepo wa bato ya ufungaji baina ya Fei Toto na Azi Ki, kwani inawafanya mastaa hao wawe na morali ya kutamani kufunga kila mechi, ingawa wakati mwingine inaibua presha, inapotokea mwingine kamzidi mabao mwenzake.
“Nimekumbuka ilivyokuwa kwangu na Mayele, kama Mtanzania natamani Fei Toto achukue kiatu italeta heshima kwa wazawa, baada ya msimu uliopita tuzo hiyo kwenda kwa wageni,” alisema Mpole ambaye timu yake ya FC Lupopo ipo katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya DR Congo.
Alisema anachokionyesha Fei Toto kinaleta heshima ya thamani za wazawa.
Hoja yake Mpole iliungwa mkono na staa wa zamani wa Simba, Yanga na Stars, Haruna Moshi ‘Boban’ aliyesema Fei Toto ni kati ya wazawa wanaofanya vizuri “Ingawa mechi za mwisho zitaamua nani anastahili kunyakua kiatu cha dhahabu, ila Fei Toto ni kati ya viungo bora katika nchi hii.”
Kwa upande wa Fei Toto alisema;”Nafunga kwa ajili ya timu yangu kufikia malengo yake, siwezi kushindana na mtu mwingine, kuhusu tuzo ya ufungaji bora naitamani.”
Msimu uliopita Aziz Ki alimaliza na mabao tisa, wakati Fei Toto alimaliza akiwa na mabao sita, hivyo 2023/24 umekuwa wa mafanikio makubwa kwao.