Basi la Takbir lapata ajali Singida

Singida. Basi la kampuni ya Takbir lililokuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Geita limepata ajali na kujeruhi watu 18.

Ajali hiyo imetokea alfajiri ya leo Mei 23, 2024 eneo la Manga lililopo Wilaya ya Singida mkoani Singida.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Singida, Amon Kakwale amezungumza na Mwananchi leo kwa njia ya simu na kuthibitisha kutokea kwa ajali hiyo.

Hata hivyo amesema hakuna kifo hata kimoja hadi sasa, ingawa majeruhi ni wengi na bado hajapata idadi yao.

“Chanzo bado hakijafahamika lakini hakuna kifo hata kimoja hadi sasa zaidi ya majeruhi ambao bado hatujapata idadi yao ingawa ni wengi,” amesema kamanda huyo.

Kwa mujibu wa mashuhuda, kabla ha kutokea kwa ajali, basi hilo lililikwepa gari dogo lililokuwa limeegeshwa pembezoni mwa Barabara, kisha likaanza kuyumba na kugonga karavati na kupinduka, likigeukia lilikotoka.

Kwa upande wake, Manase Juma amesema basi lilimshinda dereva baada ya kukwepa gari lililokuwa kando ya barabara, ndipo likapinduka.

“Tunaomba hawa wanaogesha kwenye hii sehemu watafute sehemu nyingine, kwa ssababu si mara ya kwanza, kuna siku pia gari liliingia hapa, kungekuwa na watu yangetokea maafa, hii sehemu ya packing si salama,” amesema.

“Baada ya ku-overtake, basi likamshinda dereva, likagonga ile ngema, likaanguka, likageuka lilipotokea, tukapiga simu polisi wakaja tumeshuhudia majeruhi ila hatujaona waliokufa,” amesema.

Baadhi ya majeruhi katika ajali hiyo wamesema safari ilianza majira ya saa 2 usiku jijini Dar es Salaam na dereva alikuwa na mwendo wa kawaida, ingawa walichokishuhudia ni basi kuyumba mara tatu na kuanguka.

Akizungumza tukio hilo, Faida Bilii aliyekuwa siti namba 16 akielekea Katoro, Geita amesema anadhani dereva alikuwa anasinzia kwa sababu alichokishuhudia ni gari kuyumba mara tatu kisha kuanguka.

“Mwendo njiani ulikuwa wa kawaida, sasa nadhani dereva alikuwa na usingizi, gari liliyumba mara tatu likaanguka,” amesema Faida.

Naye Benjamin Batlomeo amesema alikuwa amelala na kilichomwamsha ni basi hilo kuyumba kwa takriban dakika moja na ghafla wakajikuta wamepinduka.

Related Posts