Ihefu yamnyatia Waziri Junior | Mwanaspoti

VIONGOZI wa Ihefu, wamevutiwa  na kiwango anachokionyesha mshambuliaji wa KMC, Waziri Junior na tayari wameanza mazungumzo naye, kama watafikia mwafaka huenda msimu ujao akawa sehemu ya kikosi chao.

Junior ambaye msimu uliopita alimaliza na bao moja alifunga dhidi ya Geita Gold, Ligi Kuu inayoendelea amekuwa na kiwango kizuri hadi sasa anamiliki mabao 12 na asisti moja.

Habari za ndani zinasema kati ya washambuliaji wazawa waliopewa ofa na Ihefu ni Junior ambaye anamaliza mkataba wake msimu huu.

“Tayari tumempa ofa yetu, alihitaji muda wa kuichambua na kuingalia kama inamfaa, kutokana na kiwango chake, tunashawishika kuwa naye msimu ujao,” alisema kiongozi huyo.

Alipotafutwa Junior alisema amepokea ofa nyingi, lakini maamuzi ya atakwenda wapi itakuwa baada ya kumaliza mechi zilizobakia, ili kuisaidia timu yake kuyafikia malengo.

“Kama umesikia Ihefu inanihitaji basi itakuwa kati ya timu ambazo zimekuja kuniletea ofa zao, ila kipindi hiki siyo cha kuweka nguvu huko, hadi tutakapomaliza msimu nitapata muda wa kujua naamua kipi,”alisema.

Msimu wa 2015/16 akiwa na Toto Africans,  mabao saba, 2016/17 (Toto)  mabao 7, 2017/18 bao moja (Azam FC),  2018/19 (Biashara United) mabao matatu, 2019/20  mabao 13 (Mbao FC) pray-off mabao 2,  2020/21  mabao mawili (Yanga), 2021/22  mabao manne (Dodoma Jiji), 2022/223 bao moja (KMC) na 2023/24 mabao 12 (KMC).

Related Posts