WANANCHI wa Kata ya Kivule Mtaa wa Magole A, jijini Dar es Salaam, wameonesha kutoridhishwa na hatua ya barabara ya Nyang’andu kujengwa kwa kiwango cha udongo badala ya changarawe ili iweze kutumika katika nyakati zote. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Malalamiko hayo yameibuliwa leo tarehe 23 Mei 2024, siku chache baada ya barabara hiyo kumwagwa kifusi cha udongo, kinyume na maombi ya wananchi waliotaka kijengwe kwa changarawe wakati ikisubiri lami.
Akizungumza kwa niaba yao, Mwanaharakati huru, Bihimba Mpaya, amesema uamuzi huo hautasaidia kuwaondoa wananchi katika adha ya usafiri wanayoipata kutokana na barabara hiyo kuwa korofi hasa wakati wa mvua.
“Hii barabara badala ya kumwagwa kifusi cha changarawe chenye mawe wenyewe wanamwaga tope la udongo hapa umefanyika ufisadi mkubwa kupitia fedha za wananchi,” amesema Bihimba na kuongeza:
“Tunaiomba Serikali itekeleze maombi ya wananchi ili barabara hii ijengwe kwa changarawe ili iweze kupitika kwa muda wakati tunasubiri lami. Wakati wa mvua barabara haipitiki kabisa sasa Serikali imetoa pesa kuweka changarawe badala yake wameweka udongo.”