Jubilee Insurance yawakumbuka watoto wenye utapiamlo

Dar es Salaam. Katika kurudisha kwa jamii Kampuni ya Bima ya Jubilee Allianz General imetoa msaada wa vifaatiba katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala iliyopo Kinondoni Dar es Salaam.

Vifaa vilivyotolewa ambavyo vimeelekezwa moja kwa moja kuwahudumia watoto wenye ugonjwa wa utapiamlo ni pamoja mfuko wa sukari, viti 15, maziwa maboksi matatu, sinki pamoja na mzani wa kuwapimia watoto hao.

Akipokea msaada huo uliotolewa jana Jumatano ya Mei 22, 2024, Ofisa Muuguzi Kiongozi Hodi ya Watoto katika hospitali hiyo, Atila Mpwage amesema vifaa hivyo vitawasaidia katika kuwapa huduma watoto hao wenye upungufu wa lishe.

“Tunashukuru kwa vifaa hivi, kama hii sukari tunatengeneza tibalishe kwa ajili ya maziwa, mzani pia utatusaidia kuwapima ili kujua namna ya kutoa tiba kulingana na uzito wao,” ameeleza.

Aidha, amesema huwa inatokea changamoto ya upungufu sukari, na hata mzani pia hivyo msaada huo una maana kubwa katika ustawi na maendeleo ya watoto hao.

Wakati Mpwage akiyaeleza hayo, Florence Uledi, muuguzi kiongozi wa zamu amesema uongozi wa hospitali hiyo umepokea kwa mikono miwili vifaa hivyo vyenye umuhimu.

Uledi, ambaye amemwakilisha Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, amehimiza na kampuni nyingine kutoa misaada kwa wenye mahitaji kwani ni jambo lamsingi.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Jubilee Allianz General Insurance Company, Dipankar Acharya amesema wamekuwa na desturi ya kurudisha kwa jamii, ikiwa ni sehemu ya malengo yao kama kampuni.

“Ni tukio la furaha kwetu na siku zote tumekuwa tunaamini katika utamaduni huu wa kujiweka karibu na kurudisha kwa jamii,” amebainisha Acharya.

Ameongeza kuwawanamini katika ustawi wa jamii na hata katika matukio mengine wamekuwa wakitekeleza usafi ikiwemo kusafisha fukwe za bahari na hata masoko.

Related Posts