Baraza la Usalama AU kuwakutanisha vigogo Tanzania

Dar es Salaam. Viongozi mbalimbali wakiwemo marais wastaafu wanatarajiwa kuhudhuria maadhimisho ya miaka 20 ya Baraza Usalama na Amani la Umoja wa Afrika, yatakayojadili pia kuhusu hali ya ulinzi na usalama barani humo.

Miongoni mwa washiriki ni Waziri Mkuu wa zamani wa Chad, Moussa Faki Muhammad ambaye ni mwenyekiti wa kamisheni ya Umoja wa Afrika, Makamu wa Rais wa Uganda, Jesca Alupo, Rais mstaafu wa Nigeria, Oluṣẹgun Ọbasanjọ.

Wengine ni marais wastaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete, Domitien Ndayizeye (Burundi) Joaquim Chissano (Msumbiji), pia atakuwepo waziri wa mambo ya ndani ya Msumbiji.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba ameeleza hayo jana Jumatano Mei 22, 2025 wakati akizungumza na wanahabari kuhusu maandalizi ya maadhimisho hayo yatafanyika Mei 25, 2024 katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam ambapo Tanzania inashirikiana na Kamisheni ya Umoja wa Afrika.

Waziri Makamba amesema Rais Samia ameridhia maadhimisho hayo baada ya kushauriana na kamisheni ya Umoja wa Afrika, kwamba ifanyike shehere kubwa jijini Dar es Salaam, itakayoshirikisha marais kadhaa, viongozi wakuu wastaafu na kamisheni ya Umoja wa Afrika.

“Kutakuwa na mhadhara siku hiyo, mazungumzo na majadiliano utakaoendeshwa na jopo la viongozi wastaafu na viongozi wengine watakaojadili kaulimbiu ya maadhimisho haya ya miaka 20 ya Baraza la Amani na Usalama, likiwa chombo cha uamuzi, miongo miwili ya Afrika, amani, usalama tunaoutaka.

“Kutakuwa majopo mawili yatakayojadili hali ya ulinzi na usalama Afrika kwa miaka 20 iliyopita na mwelekeo kwa miaka ijayo,” amesema Waziri Makamba.

Baraza la Amani na Usalama Bara la Afrika ni chombo kikuu katika Umoja wa Afrika chenye jukumu la kuzuia, kusuluhisha migogoro. Chombo hicho kilianzishwa Mei 25, mwaka 2024.

Amefafanua kila mwezi chombo hicho kinakuwa na mwenyekiti wa baraza hilo na Mei mwaka huu, Tanzania ndiyo mwenyekiti wake.

Waziri Makamba amesema kuelekea Mei 25 wamekuwa wakifanya shughuli mbalimbali zilizofanyika kila wiki ikiwemo usuluhishi, misaada na mahitaji ya kibinadamu, nafasi ya wanawake na vijana katika ulinzi na usalama na kusaidia misheni za amani.

Waziri Makamba amesema Tanzania imekuwa na historia kipekee katika bara la Afrika kuhusu amani, ulinzi na usalama na kwa miaka mingi Tanzania imekuwa kitovu cha harakati za ukombozi barani Afrika.

“Wapigania uhuru wa nchi za Afrika wakati  wanatafuta uhuru wa ukombozi wa mataifa yao walitumia Tanzania kama sehemu ya kujipanga, hivyo nchi yetu inaheshimika duniani na Afrika kwa mchango wa ukombozi katika bara hili.

“Tanzania ilitoa msaada mkubwa katika harakati hizo, kuna vyama vya ukombozi vya kusini mwa Afrika vilianzishwa hapa Dar es Salaam, kuna baadhi ya viongozi wa juu wa nchi hizi wanazungumza kiswahili kwa ufasaha kwa sababu waliishia Tanzania,” amesema.

Makamba amesema baada ya ukombozi kupatikana kazi ya Tanzania iligeuka na kuwa kulinda uhuru amani na usalama wa bara la Afrika, kwa sababu hakuna faida ya kuwa nchi huru halafu hakuna usalama.

“Ndio maana katika nchi za Afrika zinazoongoza kusaidia jitihada za kupata amani barani Afrika katika ukanda huu ni Tanzania, ndio maana mazungumzo ya amani na kusuluhisha yamefanyika hapa.

“Shughuli itakayofanyika Mei 25 ni sahihi kwa Tanzania kuifanya, ndio mahala pake kwa sababu nchi yetu ni kiongozi katika kuleta amani na usalama barani Afrika,” amesema Waziri Makamba.

Related Posts