Lindi. Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack ametoa wiki mbili kwa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (Temesa) kuhakikisha unamaliza tatizo la kivuko cha Mv Kitunda ili wananchi waendelee na shughuli zao kwa uhakika zaidi.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Alhamisi Mei 23, 2024, Telack ameelekeza kivuko hicho kiache kuvusha watu kutokana na hitilafu iliyopo, inayosababisha wakati mwingine kizime kikiwa baharini.
Telack amesema baada ya kivuko hicho kukarabatiwa kwa Sh1 bilion, bado kinashindwa kuvusha wananchi kwa uhakika kutokana na hitilafu.
“Nasitisha huduma za uvushaji hadi pale kivuko kitakapokaa sawa. Mkandarasi hakikisha ndani ya wiki mbili kinarudi kwenye hali yake, leo mtatafuta njia mbadala ya kuwavusha watu, kazi ya uvushaji iendelee kama kawaida lakini mtajua wavuke na nini,” amesema Telack.
Meneja wa vivuko kanda ya mashariki na kusini, Abraham Amily amekiri kupokea maagizo kutoka kwa mkuu wa mkoa na kuahidi kuyatekeleza na kuwa kazi hiyo haitafika wiki mbili alizozitoa mkuu wa mkoa.
“Ninakiri kupokea maagizo kutoka kwa mkuu wa mkoa, nimuhakikishie hazitafika wiki mbili kivuko cha Mv Kitunda kitaendelea na kazi yake kama kawaida,” amesema Amily.
Safina Mohamed, mkazi wa Mnali amesema kivuko hicho kinasumbua kutokana na ubovu, wakati mwingine kinaweza kufika kwenye maji kikapoteza mwelekeo.
Hata hivyo, ameiomba Serikali kutositisha moja kwa moja shughuli za uvushaji abiria, bali waletewe kivuko kingine ndipo hicho kifungiwe.
“Kama wanataka kusitisha kutokana na ubovu uliopo watuletee kivuko kingine, kwani hiki hata kama kibovu kinatusaidia kuliko kupanda maboti,” amesema Safina.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Nachingwea, Sufiani Hamis amesema tatizo la kivuko ni kwamba kinaweza kufanya kazi siku moja lakini siku ya pili kikashindwa, ameitaka Serikali kuwapelekea vivuko vingine.
“Kivuko hiki unakuta leo kinavusha, kesho hakivushi, lakini kinasaidia, niiombe Serikali ijitahidi kuleta kingine kabla hawajasimamisha kabisa hiki,” amesema Hamis.
Mtumiaji mwingine wa kivuko hicho, Kais Athumani ameiomba Serikali kuwaletea kivuko kingine haraka kwa kuwa kikiondolewa shughuli za kila siku za wananchi zitaathirika.
“Huduma zote tunapata mjini, japo ni kibovu lakini kinasaidia mara moja moja kutuvusha, tofauti na kutokuwepo kabisa. Hizi boti sio salama sana kwenye uvushaji,” amesema Athumani.