WATETEZI wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), KMKM wameishusha rasmi Maendeleo baada ya jana kuifumua mabao 7-0 katika mechi ya ligi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mao A, mjini Unguja.
Ushindi huo umeifanya KMKM kuchupa hadi nafasi ya pili kutoka ya nne iliyokuwapo kwa kufikisha pointi 51, lakini kipigo hicho kimeifanya Maendeleo kusalia mkiani mwa msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 15 na kuwa timu ya kwanza kati ya nne za kushuka daraja msimu huu kwa mujibu wa kanuni.
Timu hiyo hata kama itashinda mechi nne ilizonazo kukamilisha msimu itaifanya ifikishe 27 tu zilizopitwa na baadhi ya timu zilizopo juu yake kwa sasa,kitu kinachoiingiza moja kwa moja kati ya timu nne zinazoenda na maji.
Hicho pia kilikuwa kipigo cha tano mfululizo kwa timu hiyo katika ligi hiyo ndani ya mwezi huu wa Mei, ikiwa imeruhusu jumla ya mabao 25 na yenyewe kufunga nane, kwani ilianza kwa kufungwa 4-2 na JKU, kabla ya kulala 2-1 kwa Ngome.
Pia ilichapwa kwa mabao 7-3 na KVZ kisha kufumuliwa 5-2 na Mlandege ikanyooshwa kabla ya jana kulala tena 7-0, ikiwa timu ya pili msimu huu kufungwa idadi hiyo baada ya Jamhuri ya Pemba ambayo nayo ipo katika janga la kushuka daraja iliyonyoioshwa na JKU Mei 17.
Katika mechi ya jana, watetezi wa taji hilo inayolishikilia kwa misimu mitatu mfululizo ilipata mabao kupitia kwa Ilyasa Suleiman aliyefunga bao la kwanza ya tano tu, kabla ya Ibrahim Ishaka kufunga mawili dakika za 29 na 58 na kumfanya afikishe mabao 12 msimu huu akipanda hadi nafasi ya tatu ya Wafungaji wa Ligi hiyo nyuma ya Suleiman Mwalimu wa KVZ wenye 19 na Ibrahim Hamad ‘Hilika’ wa Zimamoto aliyefunga 14.
Wachezaji wengine walioshiriki kuizamisha Maendeleo illiyopanda msimu huu sambamba na Ngome, New City na Chipukizi walikuwa ni Salum Akida Shukuru aliyefunga pia mawili dakika ya 60 na 90′ pamoja na Mzee Hassan Mzee aliyetupia dakika ya 51 na Masumbuko Ngulumbe wa Maendeleo alijifunga dakika ya 72.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mao B, pia mjini Unguja mabingwa wa zamani Mlandege waliinyoosha Jamhuri kwa mabao 2-o.
Mabao ya washindi yaliwekwa kimiani na Jamal Fadhil Ramadhan dakika ya 12 na Mussa Hassa Salum aliyetupia dakika ya 78 na kuzidi kuiweka pabaya Jamhuri iliyopo nafasi ya 15 ikiwa na pointi 18 baada ya mechi 26.
Ushindi huo ni wa saba kwa Mlandege na umeifanya timu hiyo ipande kwa nafasi mbili kutoka ya 10 hadui ya nane kwa kufikisha pointi 33 baada ya mechi 25.