Mchina chini ya ulinzi akituhumiwa kwa utapeli

Arusha. Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Felician Mtahengerwa ameagiza kukamatwa kwa raia mmoja wa China, Wang Zhiqiang ambaye anatuhumiwa kwa utapeli.

Pia, mkuu huyo wa wilaya ameliagiza Jeshi la Uhamiaji wilayani humo kushikilia hati zake za kusafiria na vibali vyote alivyonavyo raia huyo hadi atakapolipa madeni yote ya wateja wake.

Mchina huyo anatemiliki kampuni ya YBN Great Wall Garage katika eneo la Mbauda jijini Arusha, anatuhumiwa kutapeli zaidi ya Sh74 milioni kutoka kwa wateja wake.

Mtahengerwa ametoa amri hiyo leo Jumatano Mei 22, 2024 akiwa kweye kliniki ya kusikiliza kero za wananchi aliyoianza leo ofisini kwake.

Mmoja wa wateja wa Zhiqiang aliyejitambulisha kwa jina la Noel Kikwale, amedai kuwa alipeleka gari lake aina ya Mitsubishi Outlander kwenye gereji hiyo na akamtaka amtangulizie Sh21 milioni na kuwa likikamilika ammalizie Sh4 milioni, lakini mpaka sasa anamzungusha.

“Baada ya kumpatia fedha tulisainishana  mkataba Oktoba 16, 2023 kwamba ifikapo Desemba 24, 2023 atakuwa amekamilisha kazi lakini hadi leo bado halijatengemaa na amelifungua kila kitu, nikimfuatilia anatoa majibu ya kejeli,” amedai Kikwale.

Naye mmiliki wa nyumba aliyopanga Mchina huyo kwa ajili ya gereji,, Valmohamed Juma amesema anamdai kodi ya miezi 17 inayofikia Sh27.6 milioni na amegoma kuilipa.

“Mheshimiwa naomba unisaidie nipate kodi yangu na ninataka aondoke kwenye nyumba yangu maana hana faida tena, kwanza ni mkorofi lakini kila siku kwangu ni vurugu kutokana na watu wanaomdai, ambao anachukua magari yao na fedha bila kuyatengeneneza,” amedai mwenye nyumba huyo.

Akijitetea, Zhiqiang amekiri kupokea tenda za kutengeneza magari kwa watu wengi lakini anashindwa kuyatengeneza ndani ya muda kutokana na kukatiwa umeme pamoja na maji na mwenye nyumba wake.

“Nimeishi hapa Tanzania kwa muda mrefu nikifanya shughuli zangu na watu wengi kwa uaminifu mkubwa na vijana wa Kitanzania, ambao nimewaajiri, sijawahi kushtakiwa kwa kasoro yoyote, bali hivi karibuni nilipata shida nikashindwa kulipa kodi, nikakatiwa umeme na maji, huduma ambazo zinanisaidia katika shughuli zangu.”

“Naomba mkuu nisaidie kuniombea kwa mwenye nyumba wangu anirudishie umeme na maji, nifanye kazi nipate hela za kumlipa na kutengeneza magari ya watu,” amesema Zhiqiang.

Akizungumzia swala hilo, Mkuu wa Wilaya alikataa ombi lake akisema amekuwa muongo na alishawahi kuwatapeli hata wachungaji (hakuwataja majina) waliopeleka magari yao kwenye gereji yake kwa matengenezo.

“Wewe ni muongo, mimi mwenyewe nilikupigia simu juu ya gari ya mchungaji aliyekupa Sh26 milioni, lakini hujatengeneza gari lake hadi leo unapiga danadana,” amesema mkuu huyo wa wilaya.

Kutokana na hilo, Mtahengerwa ameagiza raia huyo kuwekwa chini ya ulinzi hadi atakapolipa madeni yote anayodaiwa.

Related Posts