AKILI ZA KIJIWENI: Dabo anafanikiwa hapa Azam FC

AZAM FC imejipata kiukweli dakika hizi za lala salama za ligi kuu na ingawa imeshindwa kutwaa ubingwa, ipo katika uwezekano mkubwa wa kumaliza katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 63 sawa na Simba ambayo nayo ina idadi hiyo ya pointi.

Hata hivyo, Azam iko nafasi ya pili kwa vile ina utofauti mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa na ina 36 na Simba 31.

Uwezekano wa Azam kumaliza katika nafasi ya pili na kupata tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika kwa sasa ni mkubwa na kazi imebakia mikononi mwake ya kupata ushindi wa idadi nzuri ya mabao kwenye mechi mbili zilizobakia dhidi ya Kagera Sugar na  Geita Gold ili iweze kutimiza hilo.

Wakati huohuo, timu hiyo imetinga fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania baada ya kuifunga mabao 3-0 Coastal Union kwenye nusu fainali na itakutana na Yanga, mchezo utakaopigwa Zanzibar, Juni 2.

Huwezi kutenganisha mafanikio hayo ya Azam kwa sasa na kocha Youssouf Dabo kutoka Senegal kutokana na kazi kubwa ambayo amekuwa akifanya akisaidiana na Bruno Ferry.

Kinachombeba Dabo Azam, kwanza ni kufanikiwa kujenga imani kwa wachezaji wake kuamini na kufanyia kazi kile anachokifundisha na kukielekeza tofauti na mwanzoni na inaripotiwa alitofautiana na baadhi ya nyota wa timu hiyo.

Jambo la pili sapoti kubwa anayopata kutoka kwa mabosi wa timu hiyo ambao wanahakikisha kile anachohitaji anakipata na kinatimizwa kwa haraka pasipo usumbufu na longolongo zozote.

Kuna uhusiano mkubwa kati ya mafanikio na muunganiko mzuri wa pande hizo tatu kwa maana ya wachezaji, viongozi na benchi la ufundi na ndio maana unashuhudia leo kazi ya Dabo inaonekana rahisi.

Related Posts