Mchengerwa aagiza Tarura wapatiwe Sh250 milioni

Morogoro. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Tamisemi, Mohamed Mchengerwa amemuagiza Katibu Mkuu kuipatia Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (Tarura) Sh250 milioni za dharura kwa ajili ya kujenga daraja la muda la Mbuga katika mto Luhombero pamoja na ukarabati wa daraja la waenda kwa miguu la Chigandugandu wilayani Ulanga, Mkoa wa Morogoro yaliyoharibiwa kutokana na mafuriko.

Ametoa maagizo hayo jana Jumatano, Mei 22, 2024 wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Mwaya na Mbuga ambao hivi sasa hawana mawasiliano na inawalazimu kutumia mtumbwi wa kuvutwa kwa Kamba. Yeye mwenyewe Waziri Mchengerwa ametumia usafiri huo kuvushwa.

“Ndugu zangu kwanza tupate daraja la muda litakalowawezesha wananchi kupita wao wenyewe pia kupitisha mazao yao katika msimu huu wa mavuno, hatuwezi kutimiza malengo yetu kama daraja hili bovu,” amesema.

Waziri Mchengerwa amesema kwa siku tatu za ziara yake kwenye wilaya zilizopata mafuriko mkoani Morogoro ameshuhudia maeneo mengi yaliyopata uharibifu mkubwa wa miundombinu na kumuagiza Katibu Mkuu kuipatia Tarura Sh250 milioni.

Pia, ametoa maelekezo kwa Tarura kuanza mara moja mchakato wa dharura wa ujenzi wa daraja hilo na kuwapa mwezi mmoja na nusu kulikamilisha. Amewasıhi wananchi kuendelea kufanya kazi kwa bidii ikiwemo shughuli za kilimo kwani Rais Samia Suluhu Hassan anaendelea kuwajali na kuiangalia Ulanga hususani kwenye miundombinu.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima amesema daraja hilo ni la kiuchumi, kwani wakulima walikuwa wanatumia mtumbwi kuvusha mazao yao.

Amesema ni vyema kuanza kujenga vivuko vya muda katika mkoa wake ili kuweza kuwavusha wananchi na mali zao wakati wanasubiri kujengewa daraja la kudumu.

Awali, Mbunge wa Ulanga, Salim Hasham amesema kata ya Mbuga ina watu wengi na ndio inayoongoza kwa uzalishaji pamba na ufuta, ambapo inaifanya Mahenge kuwa na zao la biashara.

Amesema licha ya matatizo ya Ulanga ni makubwa ila tatizo la daraja hilo ni kubwa zaidi  na amemshukuru Waziri Mchengerwa kufika eneo hilo ambalo wananchi wa kata ya Mwaya na Mbuga walikuwa wakipata adha ya usafiri hususani wagonjwa.

Naye Diwani wa Mbuga, Said Mfaume amesema daraja hilo litakuwa mwarobaini wa kuwasaidia wananchi wa kata yake, kwani wanazalisha  mazao ya chakula na  biashara kwa asilimia 75 pia wakazi hao hupata huduma za afya upande wa pili wa Kata ya Mwaya.

Related Posts