Longido. Baadhi ya wanawake wanaojifungua katika Zahanati ya Leremeta iliyopo Kijiji cha Sinya, wilayani Longido, Arusha wanalazimika kupewa taka zitokanazo na uzazi wao ‘kondo’ kwa ajili ya kwenda kuziteketeza majumbani kwao.
Kukosekana kwa chemba ya kichomeo taka kwa kutuo hicho ni sababu ya wanawake hao kukutana na magumu hayo. Na kuna wakati wataalam wa afya hulazimika kuchimba shimo na kufukia taka za baadhi ya wazazi wanaokataa kuondoka nazo.
Utamaduni huo usiokubalika unaendelea katika kituo hicho kilichogharimu zaidi ya Sh88 milioni na kuanza kutoa huduma mwanzoni mwa mwaka huu na kina watoa huduma wawili ambao ni Ofisa Muuguza Msaidizi na Ofisa Tabibu.
Hayo yamebainishwa leo Alhamisi Mei 23, 2024 na Ofisa Muuguzi Msaidizi wa Kituo hicho aliyejitambulisha kwa jina moja la Nurdeen, katika ziara ya siku ya kwanza ya Mkuu wa Mkoa huo, Paul Makonda aliyoanza leo wilayani hapo.
“Changamoto kubwa inayotukabili hapa ni kutokuwa na chemba ya kuchomea taka zikiwemo taka za uzazi, hali inayotulazimu kuwapa baadhi ya wazazi wanaojifungulia kituoni hapa taka hizo kwa ajili ya kwenda kuziteketeza majumbani na wanaokataa kuondoka nazo tunazifukia kwenye mashimo,” amesema.
Ofisa huyo amesema zahanati hiyo iliyopo katika Kijiji cha Sinya, inakabiliwa na changamoto nyingine ambazo ni maji, umeme hali inyosababisha kutumia majiko yao binafsi ya gesi na kusafisha vifaa tiba kwa kuvichemsha.
“Kwenye zahanati hii ni chumba kimoja pekee kina umeme na umeme wake ukichomeka hata chaja ya simu unazima, kwa hiyo tunalazimika kutumia majiko yetu ya gesi kusafisha vifaa tiba baada ya kuhudumia wagonjwa na pia umeme mdogo unasababisha hata kipimo kidogo cha damu kushindwa kufanya kazi,” ameongeza.
Ofisa huyo ametaja chanagmoto nyingine ni kutokuwa na mtu wa kufanya usafi hali inayowalazimu watumishi hao kufanya usafi ndani na majengo ya zahanati hiyo pamoja na maeneo ya nje ikiwemo kufyeka nyasi kutokana na viongozi wa kijiji na kamati ya afya kutotoa ushirikiano.
Akijibu changamoto ya umeme, Meneja wa Tanesco wilaya ya Longido Mhandisi Lazaro Lenoi, amesema waliunganisha umeme mdogo wa njia moja katika zahanati hiyo kutokana na maombi yaliyowasilishwa.
“Mkuu wa mkoa uongozi ulilipia umeme mdogo wa njia moja lakini wakilipia umeme mkubwa wa njia tatu hata kesho tutawafungia huo umeme,” amesema.
Kutokana na adha hiyo, Makonda ametoa fedha zaidi ya Sh100,000 kwa ajili ya kuunganisha umeme wa njia tatu na kufungwa katika kituo hicho ndani ya siku tatu ili huduma zitolewe kwa usahihi.
Mmoja wa kinamama wa kijiji hicho, Neema Mollel amekiri ni kweli baadhi ya wanawake wanaojifungulia hapo wamekuwa wakiondoka na taka za uzazi jambo ambalo linaweza kuhatarisha usalama wao.
Katika hatua nyingine, Makonda amememtaka Meneja wa Wakala wa Maji Safi na Usafi wa mazingira Vijijini (Ruwasa), Wilaya ya Longido, Mhandisi Ramadhan Musiba, kuandika barua kwa Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri kumueleza makosa yake ya kumdanganya mbele ya wananchi na kushindwa kufuatilia miradi ya maji.
Makonda ameonya baadhi ya watendaji mkoani humo kutotembelea miradi ya maendeleo wanayotekeleza katika maeneo yao jambo, ambalo limekuwa likichangia wananchi kukosa huduma muhimu ikiwemo maji,umeme na barabara.
Mkuu huyo amemueleza mtendaji huyo kuwa sababu za kuandika barua hiyo ni kusema uongo na kumdanganya mbele ya wananchi kuhusu ubovu wa miundombinu na kutoutembelea mara kwa mara na kusababisha wananchi kutokuwa na maji.
“Mtafute Katibu Mkuu wizara ya maji kwa kumuandikia barua umwambie kwamba Makonda hanitaki kwa sababu nimesema uongo na nimemdanganya mbele ya wananchi,” amesema Makonda.
Hatua hiyo inakuja, baada ya mwenyekiti wa Kijiji hicho, Supuk Lanyore, kumweleza mkuu huyo kuwa wamekuwa na changamoto ya maji katika zahanati hiyo, kwa zaidi ya miezi mitatu hali inayosababisha wananchi kukosa huduma ya maji.
“Zaidi ya miezi mitatu nimemuambia mhandisi kwa simu na nikaenda hadi ofisini kwake, nikamuandikia barua lakini hakujibu chochote,”amesema.
Hoja hiyo ya Mwenyekiti iliungwa mkono na mmoja wa wananchi wa kijiji hicho, Laizer Melita, ambaye ameeleza mabomba yamepasuka kwenye viungio kunavuja maji na kuwa walitakiwa kujengewa vilula vitano lakini wamejengewa viwili.
Ameeleza Septemba mwaka jana, aliyekuwa Naibu Waziri wa Maji kwa wakati huo Mhandisi Maryprisca Mahundi, alitembelea mradi huo ambao ulielezwa kufikia asilimia 90.
“Hatujawahi kumuona Mhandisi kwa miezi saba na kuwa jana majira ya saa mbili usiku tulimuona akipita akiwa na bodaboda,” amedai.
Hata hivyo, madai hayo yalijibiwa, Mhandisi Musiba, aliyesema tuhuma hizo za wananchi siyo za kweli na kwamba ametembelea mradi huo wiki mbili zilizopita na alipobanwa zaidi alikiri kuwa hajatembelea mradi huo kwa muda na akakiri ni kweli kuna upotevu wa maji kutokana na miundombinu kwenye viungio vya mabomba kuvuja.