TRA yawang’ang’ania wafanyabiashara Mbeya | Mwananchi

Mbeya. Wakati wafanyabiashara wakifunga maduka katika Soko la Mwanjelwa jijini Mbeya kwa madai ya kukithiri kwa utitiri wa kodi na unyanyasaji, Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) mkoani Mbeya imesisitiza kuwa itaendelea kuchukua hatua kwa wanaokiuka utaratibu.

Leo Mei 23, 2024 wafanyabiashara hawakufungua wakidai kutoridhishwa na utaratibu wa ukusanyaji mapato, wakidai kuwa wanabambikiziwa tozo nyingi, baadhi yake zikiwa nje ya utaratibu.

Mbali na kodi na tozo kama ile ya Ongezeko la Thamani (VAT), leseni ya biashara, ushuru wa huduma na usafi, mengine wanayolalamikia ni manyanyaso kutoka kwa maofisa wa TRA wakati wakikusanya kodi, kwamba wanafungiwa maduka na kunyang’anywa mizigo.

Wafanyabiashara hao wameomba kukaa na Rais Samia Suluhu Hassan na Wizara za Fedha na Mipango ili kujadiliana namna ya kuondoa changamoto zilizopo ili kila upande upate haki yake.

Akizungumzia mgomo huo leo Mei 23, 2024, Meneja wa TRA Mkoa wa Mbeya, Musiba Shaban ame wataendelea kuchukua hatua kwa wanaokiuka utaratibu.

Amesema hadi sasa Mbeya inafanya vizuri kwenye ulipaji kodi hadi kuvuka malengo, lakini baadhi ya wafanyabiashara wanakiuka utaratibu ikiwamo kukwepa kutoa risiti sahihi.

“Mfano, tuna kesi hapa, mfanyabiashara mmoja ameuza suruali ya Sh30,000 kwa Sh140 kwa maana hiyo kitu kama hicho kwa mujibu wa sheria haikubaliki na lazima tumuhoji na atueleze amenunua wapi,” amesema na kuongeza.

“Kuna wengine wanauza vifaa vya kielektroniki, anauza TV ya Sh1.2 milioni, lakini anaandika ya Sh150, 000 (kwenye risiti ya kutembelea barabarani), zipo changamoto hizo,” amesema Shaban.

Meneja huyo amesema sheria inahitaji unapouza au kununua lazima utoe au udai risiti halali na kwamba wapo baadhi hawatoi kabisa, hivyo TRA haitasita kuchukua hatua.

Amesema Aprili 23, 2024 alikutana na jumuiya ya wafanyabiashara Mbeya na kukubaliana kila mmoja kutoa risiti, lakini bado suala hilo halitekelezwi kwa baadhi.

“Wapo kama mama lishe, unapoenda kula saa 9 mchana, ukiomba risiti unapewa ya kwanza, sasa unajiuliza inakuwaje, nisisitize tunahitaji utaratibu ufuatwe kwa mujibu wa sheria,” amesema Shaban.

Shaban amewaomba wafanyabiashara kutokata tamaa badala yake wenye changamoto yoyote wafike ofisi za mamlaka hiyo kuwasilisha matatizo ili wawe salama.

“Kama sheria inavyotaka, tukimkamata mtu hajatoa risiti adhabu ni Sh1.5 milioni au asilimia 20 ya mzigo, kwa mteja asipodai risiti akikamatwa analipa Sh30,000 au asilimia 20 ya kodi iliyokwepwa,” amesema meneja huyo.

Kwa upande wake, Meya wa halmashauri ya Jiji la Mbeya, Dourmohamed Issa amesema hajui llolote kuhusu mgomo huo kwa kuwa yupo katika ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya Tactic.

“Kwa sasa siwezi kuzungumza chochote kwani sijaelewa kama kuna mgomo, nikitoka huku nitakupa taarifa kamili,” amesema meya huyo.

Akizungumzia tofauti zao na TRA, mfanyabiashara, Fredrick Shayo amesema kumekuwepo na matukio ya wafanyabishara kukamatwa na kunyang’anywa mizigo yao, hali ambayo inawafanya kuonekana tofauti na Serikali.

“Manyanyaso kwenye biashara hayapendezi, hatutendewi haki, tunanyang’anywa mizigo tunafanywa kama si Watanzania, mwisho tunaonekana hatuipendi nchi yetu, tunaomba kuwepo usawa ili nchi ichukue kodi na sisi tubaki na kitu,” amesema Shayo.

Kwa upande wake, Noah Uswege amesema wameamua kugoma kutokana na kamata kamata ya TRA kwa wafanyabiashara na kushauri kuwepo utaratibu kwa wafanyabiashara kuondoa changamoto hizo.

“Sisi wafanyabiashara wadogo hatupendezwi na migomo kwa sababu tunayo majukumu, watu wanatugemea, hivyo TRA wabadilike, Serikali ikae na wafanyabiashara kumaliza hili,” amesema Shayo.

Naye Winfrida Dickson ambaye amesafiri kutoka Tukuyu kufuata mzigo Mwanjelwa, amesema wamekerwa na mazingira waliyokutana nayo akieleza kuwa TRA wamekuwa kero kwa wafanyabiashara mkoani humo.

“Tunapozungumza nao hawatuelewi, hata kuangalia uhalisia wa maisha yalivyo, kwa sasa biashara ni ngumu kila unapoenda wao ndio wanatajwa kuwa sababu, wabadilike,” amesema Winfrida.

Hata hivyo, mwenyekiti wa wafanyabiashara hao, Aisea Mwasamala amesema hajajua sababu za mgomo huo lakini huenda wafanyabiashara hawajakubaliana na mwenendo huo.

“Tulishakaa kikao cha ndani na Meneja TRA na RPC, Mei 7, 2024, hivyo nadhani mrejesho tuliowapa hawakukubaliana nao, lakini ndiyo najiandaa kufika ili kujua sababu zaidi,” amesema Mwasamala.

Naye mwenyekiti wa soko hilo, Adam Mwakatumbula amesema utaratibu unaotumika na TRA katika kukusanya mapato si mzuri, akidai kuwa muda mwingine ni kama kudhalilishana.

“Mtu ana mtaji wa Sh5 milioni, TRA wanahitaji mapato yake, tofauti na kujadiliana na mamlaka kukadiriwa kulingana na uwezo wake, hali hii inakatisha tamaa na kupunguza nguvu” amesema Mwakatumbula.

Related Posts