Mbeya. Halmashauri ya Jiji la Mbeya limeiagiza Kampuni ya Cico kuwaondoa maneja mradi, Penfeng Wang na Mkandarasi Mshauri, Jofrey Kanjanja kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao na kusababisha miradi kusuasua.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Alhamis Mei 23, 2024 ofisini kwake, Meya wa Jiji la Mbeya, Dourmohamed Issa amesema wamelazimika kuchukua hatua hiyo baada ya kufanya ziara na kubaini miradi inayotekelezwa na kampuni hiyo inasuasua bila sababu za msingi.
Miradi inayotekelezwa na kampuni huyo ni pamoja na ujenzi wa barabara tano zenye urefu wa kilometa 12.3, ujenzi wa mifereji ya kupitisha maji ya mvua (kilometa 6.4) na mifereji inayojengwa katika jengo la maabara ya udhibiti ubora.
Issa amesema miradi hiyo imeelekezwa na Serikali kupitia Mradi wa Uboreshwaji wa Miundombinu ya Miji (TACTIC) kwa thamani ya Sh21 bilioni na ilianza Novemba 2023.
“Sijarishidhwa na utekelezaji, nimeagiza Kampuni ya Cico kuwaondoa meneja mradi na mkandarasi mshauri ili kufanya mabadiliko yatakayoleta tija,” amesema.
Amesema ni jambo la kushangaza Serikali imetoa fedha tangu Novemba mwaka jana mpaka kufika jana Jumatano Mei 22,2024 alipofanya ziara, hakuna kitu kilichofanyika huku ikitarajiwa miradi yote iwe imekabidhiwe ifikapo Februari 2025.
Meya amesema miundombinu iliyokuwa ijengwe ni barabara ya Kalobe – Itende na Machinjioni, nyingine ni Mapelele-Kabwe, Sido Mpaka Iziwa ambayo utekelezaji wake hauridhishi ukilinganisha na fedha zilizotolewa.
Amesema amemuagiza Mhandisi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Leonard Mohosea kufuatilia mwenendo wa mradi huo na kuwasilisha taarifa ofisini kwake.
Mwananchi Digital ilizungumza na Meneja mradi wa Kampuni ya Cico, Penfeng Wang ambaye amesema ameihakikishia Serikali kuwa wataongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huo na kuongeza vitendea kazi ikiwemo mitambo na wafanyakazi ili mradi ukamilike kama walivyokubaliana.
Mhandisi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Leonard Mohosea naye amesema atahakikisha anafuatilia mradi huo kwa karibu sambamba na kuweka msukumo kwa kampuni ya Cico ili mradi ukamilike kwa wakati.