Unguja. Wakati wadau wa habari wakishinikiza Serikali kukamilisha mchakato wa sheria ya huduma za vyombo vya habari, yenyewe imesema umefikia hatua nzuri na umefika kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na wakati wowote utafika Katika Baraza la Wawakilishi kujadiliwa.
Hayo yamebainika wakati wa maadhimisho ya siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari mwaka 2024 ambapo kwa Zanzibar yamefanyika leo Alhamisi Mei 23, 3024.
Katika mkutano huo uliokutanisha wadau wa habari, wanaharakati na Serikali, Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa – ZNZ), Dk Mzuri Issa amesema umefka wakati sasa Zanzibar kuwa na sera na sheria za habari zinazokwenda na mazingira yaliyopo sasa.
Zanzibar inatumia sera ya habari ya mwaka 2006 na Sheria ya huduma za vyombo vya habari ya mwaka 1988.
“Tangu mwaka 2008 tumepitia sheria hii na tunazungumza mabadiliko yake lakini zinakwama, sasa ifike wakati kwa kweli sheria hizi zibadilike,” amesema Dk Mzuri.
Amesema sheria hiyo inalenga kudhibiti vyombo vya habari na kumpa waziri mamlaka makubwa ya kuvisimamia.
“Haiwezekani kuwa na sheria za udhibiti mpaka sasa, ukitaka kufanya usajili wa gazeti lazima waziri aamue, asipotaka huwezi kufanya hivyo. Kwa kweli katika mazingira haya hatuwezi kwenda kwa wakati huu tunapozungumza utawala wa demokrasia,” amesema.
Amesema ulizi wa habari na mazingira ya habari kwa Zanzibar bado yapo chini.
Katibu Mtendaji wa Tume ya Utangazaji Zanzibar, Suleimana Salim Abdalla amekiri sheria hiyo kuwa ya zamani na kwamba mchakato wa mabadiliko ya sheria unahitaji utashi.
“Lakini habari njema ni kwamba sheria hiyo kwa sasa ipo kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na itafika barazani kujadili kwa hiyo tushirikiane kujadili, na Serikali haifurahi kuona kila siku inalamikiwa kuhusu sheria,” amesema Abdallah.
Kuhusu sera ya huduma za habari, katibu huyo amesema ipo tayari, kilichobaki ni uzinduzi wake.
Hata hivyo, amesema uhuru wowote lazima uwe na mipaka na kuwataka waandishi kujikita kwenye taaluma badala ya kutumia mihemko, jambo ambalo linaweza kuhatarisha amani ya nchi.
“Tusiwe na dhana kwamba Serikali ipo kwa ajili ya kudhibiti, inachokifanya ni kuratibu na kuhakikisha kuna mambo hayaendi tofauti na inapotokea hivyo lazima wahusika washughulikiwe,” amesema.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Ernest Sungura amesema bila kuwa na sheria nzuri, utendaji kazi wa mwandishi wa habari unakuwa katika hali ngumu.
Naye makamu Mwenyekiti wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Dk Yussuf Khamis amesema “Tunapopigania uhuru lazima uendane na mabadiliko ya kiutendaji na kubadilika. Waandishi lazima tujitathimini kuhusiana na habari zetu tunazoandika, lazima tuwape watu kile wanachokitaka na sio tunachokitaka sisi.”