WAKATI mabosi wa Simba wakisisitiza kwamba beki wa kati wa timu hiyo, Henock Inonga ana mkataba hadi mwakani na kwa sasa wanasubiri kupokea ofa kutoka klabu yoyote inayomhaji, beki huyo raia wa DR Congo ameweka bayana kwamba ‘ndo imetoka hiyo’, kwani anamaliza mkataba mwishoni mwa msimu huu.
Kumekuwa na sintofahamu baina ya Inonga na Simba, kwani ghafla tu mchezaji huyo amesepa zake klabuni baada ya kudaiwa kupata majeraha na kutotumika kwenye mechi kadhaa za Ligi Kuu, ikielezwa ameenda Ufaransa akijiandaa kutua moja ya klabu ya Afrika Kaskazini iliyompa mkataba wa awali.
Hata hivyo, sakata la mchezaji huyo aliyekuwa nguzo katika ukuta wa Simba kwa misimu mitatu mfululizo, linadaiwa lilianza tangu baada ya Dabi ya Kariakoo ya Novemba 5 ambapo Simba ilinyukwa mabao 5-1 na ile ya marudiano kuumia dakika chache na kumpisha Hussein Kazi aliyesababisha penalti ya bao la kwanza.
Habari za ndani zinasema kuwa, Inonga anajiandaa kuanza maisha mapya nje ya Msimbazi na hii ni baada ya mabosi wa klabu hiyo kudaiwa kumkunjulia njia ya kumtaka ailete mezxani klabu inayomtaka ili imalizane naye kwani inadai bado ina mkataba naye hadi mwaka 2025.
Mwanaspoti liliwasiliana na mchezaji huyo jana kutaka kujua ukweli wa mustakabali wake Msimbazi ambapo alijibu kwa kifupi kwamba mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu huu.
“Huu ni msimu wangu wa mwisho na Simba,” alijibu Inonga kwa ufupi na alipoulizwa juu ya mahali anapoibukia, aliishia tu kucheka bila kusema lolote kabla ya kukata mawasiliano na mwandishi wa habari hizi.
Hata hivyo, Mwanaspoti ilipoutafuta uongozi wa Simba ili kuweka ukweli wa ishu ya beki huyo aliyesajiliwa mwaka 2021 na Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ahmed Ally akiwa jijini Arusha kwenye amsha amsha za kujiandaa na mechi ya wikiendi hii dhidi ya KMC itakayopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, aliliambia Mwanaspoti kuwa, kama viongozi wanajua Inonga ana mkataba na klabu hiyo hadi mwakani.
“Achana na hizo habari, Inonga bado ni mchezaji wetu kwani ana mkataba hadi mwaka 2025 na kama kuna klabu inayomhitaji ni lazima ije kumalizana nasi na tumeiacha milango wazi. Simba hatuna tabia ya kumbania mtu,: alisema Ahmed.
Beki huyo aliyekuwa akiwaniwa na Yanga kabla ya kuibukia Simba misimu mitatu iliyopita, akitokea DC Motema Pembe ya DR Congo amekuwa akihusishwa na klabu ya FAR Rabat ya Morocco inayonolewa na kocha wa zamani wa Yanga, Nasreddin Nabi.
Tayari katika kujiandaa na pengo la Inonga, Simba imedaiwa imeshamalizana na beki wa kati wa Coastal Union, Lameck Lawi na ilikuwa ikimpigia hesabu nahodha wa Yanga, Bakar Mwamnyeto ambaye anamaliza mkataba wa mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa tatu mfululizo sasa iliyomsajili kutoka Coastal.