UMASIKINI WADAU WA KUCHANGIA UHARIBIFU WA MAZINGIRA NCHINI

Na Mwandishi Wetu, Morogoro

IMEELEZWA kuwa kuna uhusiano mkubwa kati ya umaskini na uharibifu wa mazingira hivyo ni muhimu wadau wa uhifadhi kuendelea kushirikiana na serikali katika kutekeleza miradi mbalimbali ya kiuchumi ili kupunguza uharibu wa mazingira.

Kauli hiyo imetolewa na Mshauri wa Maliasili wa Mkoa wa Morogoro ambaye pia ni Ofisa Wanyamapori wa mkoa huo,Joseph Chuwa,akizungumzia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya uhifadhi na Uchumi inayotekelezwa na Mfuko wa Uhifadhi wa Milima ya Tao la Mashariki (EAMCEF).

Alisema mfuko huo umelenga kuhifadhi milima hiyo ambapo wamekua wakipokea ruzuku kila mwaka kwa ajili ya utekelezaji wa miradi katika wilaya za Mlimba, Kilombero,Mvomero na Manispaa ya Morogoro zenye vijiji vinavyopakana na Hifadhi hizo.

Alisema miradi wanashirikiana katika kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo ili tija ifikiwe na kuwagusa wananchi wanaoishi pembezoni mwa milima hiyo hasa ikizingatiwa wengi wao wanaishi mazingira magumu hadi kufikika kwake siyo rahisi.

“Kuna uhusiano mkubwa sana kati ya umasikini na uharibifu wa mazingira,tusipoweza kugusa umasikini wa wale watu ili waingie katika kuhifadhi milima,hatutafika mbali na kinachotoka kwenye milima hii kinawafaa watanzania wote ikiwemo maji yanayoenda kwenye mabwawa yanayozalisha umeme,wadau tushirikiane zaidi,”alisema

Mkurugenzi wa Agriwezesha,Degracia Ignas,ambao wanatekeleza mradi wa kilimo cha uyoga kwa wanawake kwa ufadhili wa EAMCEF,alisema mradi huo unatekelezwa katika mitaa minne iliyopo Manispaa ya Morogoro ukiwemo mtaa wa Mbete Kata ya Mlimani,lengo likiwa ni kuwasaidia kujikwamua kiuchumi.

“Tukiangalia sehemu ambayo tupo tuko karibu na Milima ya Uluguru yenye vyanzo vya maji,umelenga kuhifadhi milima yetu ili isiweze kuharibika na akina mama wanasaidiwa kupata vifaa vya uzalishaji wa uyoga,mbegu,nafunzo na kuwaunganisha na masoko pindi wanapovuna,”alisema

“Tumeanza na akina mama 20 katika kila kikundi na imewasaidia kujipatia kipato kwa kipindi ambacho wameanza na kupunguza shughuli ambazo si rafiki kwa mazingira mfano kutafuta kuni kwa ajili ya kujiongezea kipato,”aliongeza

Mwenyekiti wa Kikundi cha Uyoga Mbete,Zena Feruzi,alisema kikundi hicho walianza mwaka 2022 na wameshafanikiwa kuvuna mara kadhaa na wamejiweka akiba benki na mradi huo unawasaidia kuendeleza familia zao kwa sababu wengine wameanzisha mabanda ya kilimo hicho majumbani kwao.

“Kabla ya mradi tulikuwa tunaenda msituni tunachukua kuni tunakuja kuuza,tulikuwa tunakata miti ila kwa sasa tuko na kilimo hiki.”

Naye Sikudhani Mustapha, alisema kabla ya kulima kilimo hicho maisha yalikuwa magumu kwani walikuwa wanakata miti na kuponda mawe kutoka mlimani.

Ofisa Miradi wa EAMCEF Kanda ya Kusini,Rosemary Boniphace alisema wamekuwa wakiwezesha miradi ya kilimo cha uyoga uliolenga kuwawezesha akina mama katika Manispaa ya Morogoro.

“Moja ya mikakati yetu ni pamoja na kuinua vikundi vya akina mama ambavyo vipo katika maeneo haya wanayoishi pembezoni mwa hifadhi ya milima hii,tunaamini ukimuwezesha mwanamke umeiwezesha jamii na hasa kwenye masuala ya uhifadhi na kupitia mradi huu tunawaelimisha waelewe kwanini tufanye uhifadhi na baada ya kuwapa elimu tunawaletea kitu ambacho ni mbadala wa shughuli za uharibifu wa hifadhi,”

“Akina mama hawa wengi walikuwa wanategemea wakakate kuni kule na kupasua mawe mtoni ili waweze kuendesha maisha yao ila kupitia mradi huu mbadala ni mradi rahisi,akishajenga banda na kupanda uyoga,wanasubiri kuuza ambapo huku kilo moja wanauza Sh 10,000,”alisema.

Hifadhi ya Mazingira Asilia Uluguru ni miongoni mwa hifadhi zinazopatikana katika Safu za milima ya Tao la Mashariki ambazo zimebeba hazina kubwa ya rasilimali vikiwemo vyanzo vya maji ambayo yanatumika kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati ya Taifa kwenye sekta za kilimo na nishati.


 

Mkurugenzi wa Agriwezesha,Degracia Ignas(mwenye tshirt nyeupe) akiwa na baadhi ya wanakikundi wanaojihusisha na kilimo cha uyoga mtaa wa Mbete,Kata ya Mlimani,mkoani Morogoro wakionyesha uyoga ambao uko tayari kwa ajili ya kuvunwa ambao huuzwa kilo moja kwa Sh 10,000

Related Posts