MAISHA ya wanasoka wengi yana historia ndefu. Wapo wanaoanza kwenye akademi za soka, wanaojikuta wakianza timu za mtaani na wanaoanzia shule na kutokana na vipaji vyao wanaibuka na kuwa nyota wakubwa.
Hata hivyo, wengi wanasema vipaji vyao ni tangu utotoni. Ni kweli, vipaji vingi huonekana tangu utotoni na kinapoendelezwa ndio kinakwenda kubadilisha maisha ya mchezaji na hata familia yake.
Salum Kimenya, ni kipaji kingine kilichopata umaarufu tangu akiwa shule. Tangu akiwa shule ya msingi hadi sekondari lakini ni hadi alipofika Shule ya Sekondari ya
New Era alikosomea kidato cha tano jina lake lilianza kusikika na kuimbwa shule na hapo alikuwa na umri wa miaka 17 tu.
Mwanaspoti lilimtafuta beki huyu wa Tanzania Prisons na kufanya naye mahojiano na anafunguka mengi kuhusu maisha yake ya soka ikiwamo rekodi ya kucheza muda mrefu Prison na hadi sasa ana miaka 11 akiwa na Wajelajela hao.
Kumbe akiwa shule aliupiga mwingi; Msikie;
Kimenya: Niligundua nina kipaji nikiwa Shule ya Msingi ya Mkombozi iliyoko Wilaya ya Urambo na niliendelea kucheza hata nilipojiunga na Shule ya Sekondari ya Urambo na nilipojiunga pia na kidato cha tano Sekondari ya New Era iliyopo Tabora mjini.
Hapo ndiyo kipaji changu kilizidi kuonekana. Pia nilizichezea timu za mitaani kama Chipukizi wa Umoja wa Wanafunzi Vijana wa Urambo.
Pia nilizichezea timu nyingi za mitaani kama Walumba na Twiga zote za Urambo katika ligi za wilaya na mkoa. Nilikuwa na umri wa miaka 17. Kisha nilienda Mbeya kwenye majaribio ya kucheza Tanzania Prisons, ndipo nikafaulu na kuchagua kubaki hapa na sasa nafahamika nchi nzima.
Soka likamnogea akaacha shule, kwa nini?
Kimenya: Kiukweli niliishia kidato cha tano kwa sababu ndiyo kipindi nilienda Mbeya kufanya majaribio Tanzania Prisons. Nilitarajia kama ningeshindwa ningerudi shule lakini nikafanikiwa, hivyo nikaamua kubaki niendelee na maisha ya soka, kwani ndicho nilichokipenda zaidi.
Sijawahi kujutia maana niliowaacha shule sio wote wamefanikiwa, naweza kusema Mungu alipanga nipite njia hii kwani ilikuwa ndoto yangu kucheza Ligi Kuu na timu ya Taifa.”
Kumbe alishawahi kuzikataa Simba, Azam; Msikie
Kimenya: Ni kweli, Simba na Azam kipindi hicho ziliwahi kunihitaji lakini sikuridhika na ofa zao kwani hazikunifurahisha. Nilikuwa mdogo na Prisons nimeshapata kazi, nikaona ofa ni ndogo nikaogopa kuharibu kazi yangu ya muda mrefu kwa ajili ya dili la muda mfupi. Inajulikana, timu zenye ushindani mkubwa ubora ukipungua tu na kibarua chako kimefika mwisho.”
Kimenya: Soka limenilipa kwa kweli tofauti na mwanzo nilivyokuwa. Nimefanya maendeleo makubwa na wakati huu nafanya kazi, huku nacheza mpira, pia nalima mashamba na kufanya biashara. Vyote ni kutokana na miguu yangu na maamuzi niliyofanya ya kuchagua njia hii.
Nilitamani kuwa mwanasheria, hata hiyo, niliamini nitatumia muda mrefu sana kusomea na sidhani kama kazi ningepata kiurahisi kama nilivyochagua soka. Hata hivyo, sisemi haya kukatisha tamaa wanaosomea sheria, ila nauzungumzia moyo wangu na bahati yangu kwa jumla.
Kila jambo lina changamoto zake na Kimenya kashakutana nazo hadi akatamani kuacha kucheza soka, ilikuaje?
Kimenya: Mchezaji sio vipindi vyote anakuwa sawa kiakili na kiuwezo kwa hiyo nilikuwa kwenye hali ambayo sio nzuri kiuwezo, basi kocha (hataki kumtaja) aliitumia hali hiyo kunikandamiza zaidi kwani hakuwahi kunipenda. Naweza kusema ni jambo linalotokea hata kwenye maisha ya kawaida, kuna mtu anaweza asikukubali bila kumwonyesha ubaya wowote.
Hapa sasa ndipo alipolifurahia soka. Msikie;
Kimenya: Msimu wangu mzuri zaidi katika soka ni ule niliofaya vizuri kuliko yote ni 2017/2018. Nilikuwa na asisti nyingi sana na mabao saba Ligi Kuu. Kama beki nilifanya vizuri.
Kutokana na nafasi ninayoichezea ni ngumu kufunga muda wote kama ilivyo kwa washambuliaji ambao ni kazi yao. Nilifunga mabao mengi kuwashinda wengi msimu huo.
Wengi wana ndoto za kucheza soka nje ya nchi, lakini yeye wala hana mpango, kwa nini?
Kimenya: Ndoto za kwenda nje sina. Kwanza umri umeshakwenda. Kwa sasa nitaendelea kupambana na soka la Bongo, kazi yangu na biashara zangu. Nitakuwa hapa nikisubiria kustaafu. Miaka 33 sasa sina pa kwenda, nafikiria kurudi shule kujiongezea ujuzi ili nifike mbali katika kazi.
Prisons imekuwa na msimu gani tofauti na iliyopita?
Kimenya: Kwangu naona iko sawa. Ligi ni ngumu na kila timu inafanya vizuri.
prisons hii iliwahi kushika nafasi nne za juu mara mbili ikimaliza ya nne. Kwa sasa ipo nafasi ya tano (Wakati akihojiwa, sasa hivi ni ya sita), inafanya vizuri, licha ya mwaka juzi kucheza ‘play off’.
Prisons imecheza mara moja ‘Play off’ lakini sasa iko vizuri na kwenye msimamo imecheza mechi 28 na ina pointi 33, huku ikishinda mechi saba, sare 12 na imepoteza tisa, ikifunga mabao 26 na kufungwa 29 na iko nafasi ya sita na kuhusu timu nyingine na uwekezaji kwenye soka, anasema;
Kimenya: Hata timu nyingine na uwekezaji uliofanya ni mzuri. Wadhamini wanajitahidi kuifanya ligi kuwa bora na jambo pekee ni wachezaji wenye ubora mkubwa wameongezeka kwa wingi na wote wanaofanya vizuri, nawakubali.”