JUMLA ya wagombea 14 kutoka vyama vya siasa vyenye usajili kamili wameteuliwa kuwania kiti cha Ubunge katika Jimbo la Kwahani, Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar huku vyama vikuu vya upinzani Chadema na ACT Wazalendo vikikacha uchaguzi huo. Anaripoti Mwandishi wetu, Zanzibar … (endelea).
Hatua hiyo imekuja baada ya vyama hivyo kuendeleza msimamo wa kutoshiriki chaguzi ndogo kutokana na wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi kutojiuzulu kama wanavyotakiwa na Sheria mpya ya Tume Huru ya Uchaguzi ya mwaka 2024.
Hata hivyo, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kwahani, Safia Iddi Muhammad jana Alhamisi amesema kati ya wagombea hao tisa ni wanawake na watano ni wanaume.
Safia amesema wagombea hao wote ni wale waliojitokeza kuchukua fomu na kuzirejesha ndani ya muda uliopangwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).
Fomu za uteuzi kwa ajili ya uchaguzi huo mdogo zilianza kutolewa kuanzia tarehe 17 hadi 23 Mei, 2024 ambayo pia ilikuwa siku ya uteuzi.
Safia amesema zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu za uteuzi limekwenda vizuri na amevipongeza vyama vyote vilivyojitokeza kugombea nafasi hiyo.
“Zoezi la uteuzi wa wagombea katika Jimbo la Kwahani limekwenda vizuri na tayari majina ya wagombea 14 waliojitokeza kuchukua fomu na kuzirejesha wameteuliwa kuwania kiti hicho,” alisema Safia.
Msimamizi huyo wa Uchaguzi Jimbo la Kwahani, amewataja wagombea walioteuliwa na Vyama vyao katika Mabano kuwa ni Bashir Yatabu Said (Demokrasia Makaini), Nuru Abdulla Shamte (DP), Mwanakombo Hamad Hassan (NLD), Zainab Maulid Abdallah (CCK), Tatu Omary Mungi (UPDP), Khamis Yussuuf Mussa (CCM) na Jarade Ased Khamis (AAFP).
Wengine amewataja kuwa ni Kombo Ali Juma (NRA), Shara Amran Khamis (ADC), Naima Salum Hamad (UDP), Madina Mwalim Hamad (ADA TADEA), Amour Haji Ali (SAU), Mashavu Alawi Haji (UMD) na Bw. Abdi Khamis Ramadhan (CUF).
Safia amesema tayari ameshakutana na wagombea wa Vyama vyote na wapo tayari kuanza kampeni.
Kwa mujibu wa Taarifa ya INEC iliyotolewa kwa umma na kusainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhan Kailima jijini Dodoma tarehe 2 Mei 2024 kampeni kwa ajili ya uchaguzi huo zitafanyika kuanzia tarehe 24 Mei 2024 hadi tarehe 7 Juni 2024 na uchaguzi utafanyika tarehe 8 Juni 2024.