Mwanza. Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Camilius Wambura amesema anaamini ipo siku jeshi hilo litakuwa jeshi bora duniani, huku akitaja vigezo vitatu vitakavyolifanya kufikia lengo hilo.
Wambura ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Mei 24, 2024, wakati wa hafla ya kuwavisha nishani maofisa, wakaguzi na watendaji 574 wa jeshi hilo mikoa ya Kanda ya Ziwa, iliyofanyika uwanja wa Jeshi la Polisi Mabatini na kushuhudiwa na mamia ya askari na wakazi wa jiji la Mwanza.
Waliovishwa ni sehemu ya maofisa na wakaguzi wa Jeshi la Polisi 5,607 waliotunukiwa nishani na Rais Samia Suluhu Hassan. Nishani hizo ni; Nishani ya Kumbukumbu ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, nishani ya utumishi wa muda mrefu na nishani ya utumishi wa mrefu na nidhamu nchi nzima.
Huku akiagiza utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai, IGP Wambura ametaja vigezo hivyo kuwa ni kutotenda kazi kwa mazoea, kubadilika kifikra na kuwa na msukumo wa kimaadili kwa maofisa na makamanda wa Jeshi la Polisi nchini.
“Naagiza mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai yakachambuliwe vyema na kushushwa mpaka ngazi ya chini. Yasiishie ngazi ya wilaya bali yaende mpaka kituo cha polisi kilichopo katika kata,”ameeleza.
Pia amesema Polisi litakuwa Jeshi bora duniani endapo litasimamia ipasavyo rasilimali zinazotolewa na Serikali ikiwemo majengo ya ofisi, makazi, magari na vifaa kwa kuzitumia katika ukaguzi wa kina wa miundombinu ya polisi ili itumike kwa kizazi cha sasa na kijacho.
“Ili iwe hivyo lazima tuwe na dawati la ufuatiliaji na tathmini ambazo ni makini zinazofuatiliwa kwa kina kwamba kile maelekezo yanatekelezwa kwa haki. Madawati haya ndiyo ya msingi kupima utendaji kazi yake hivyo lazima yatekelezwe kwa kina,” amesema Wambura.
Mbali na hiyo, Wambura ametaja sababu nyingine kuwa ni maofisa na wakaguzi wa jeshi hilo kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wateja kwa kutenda haki, staha, kujali muda na ubora wa huduma wanayostahili.
“Tuzingatie tunu ya utu ili kufikia lengo la jeshi la polisi bora duniani. Iko siku kwa maboresho haya yanayoendelea ndani ya Jeshi la Polisi Tanzania, jeshi letu litakuwa jeshi bora duniani,” amesema Wambura huku akidokeza kuwa ubora huo utaanzia Afrika Mashariki, Afrika na duniani kwa jumla.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa akizungumza kwa niaba ya maofisa na wakaguzi waliotunukiwa, amesema nishani hizo siyo tu zimeongeza morali, pia zimewaaongezea uwajibikaji wa kuwasimamia watendaji na kutimiza malengo ya jeshi hilo.
Amemuomba IGP na Rais Samia Suluhu Hassan kuendeleza utaratibu huo kwa wa kuwatambua maofisa waliotumikia Jeshi la Polisi kwa muda mrefu na kwa heshima.
“Siku ya leo kwetu sisi ni siku ambayo IGP na Rais Samia wametupatia heshima kubwa sana kutuonesha kwamba tunastahili nishani hizi. Inatuongezea morali, uwajibikaji na kuwasimamia watendaji wa Jeshi la Polisi tunaowasimamia kuzingatia misingi itakayotuletea mafanikio,” amesema DCP Mutafungwa.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, ameshuhudia baadhi ya askari (bila kutaja idadi) waliokiuka maadili ya jeshi hilo wakichukuliwa hatua huku akimtaka RPC Mutafungwa kutowafumbia macho askari wa aina hiyo.
Huku akidokeza kuwa kiongozi anayesimamia sheria na utaratibu hakosi minong’ono, Mtanda amewataka wakazi wa mkoa huo kushirikiana na jeshi hilo huku akiwataka kuwafichua askari watakaobainika kukiuka weledi wanapotekeleza majukumu yao.
“Nawakumbusha askari wote wenye vyeo mbalimbali kujua kwamba taasisi ya Polisi ili iwe bora lazima isimamie haki na isiwe na ukiukwaji wa maadili. Nimeona vitendo hivyo vinapojitokeza basi hatua zinachukuliwa kwa haraka, mkifanya kazi zenu kwa weledi mnastawisha na kujenga taswira ya Jeshi la Polisi,” amesema Mtanda.