Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ inatazamiwa hivi leo kutoa uamuzi juu ya ombi linaloitaka Israel kusitisha mashambulizi yake ya kijeshi huko Gaza kwa tuhuma za “mauaji ya kimbari”.
ICJ, ambayo maamuzi yake huwa ni kisheria zaidi lakini yanayokosa mifumo ya utekelezaji wa moja kwa moja, haikuamuru kusitishwa kwa mapigano katika uamuzi wake mwezi Januari lakini iliitaka Israel kufanya kila liwezekanalo ili kuzuia vitendo vya mauaji ya halaiki huko Gaza.
Soma pia: ICJ kuamua juu ya kuondoka kwa vikosi vya Israel mjini Rafah
Afrika Kusini, ambayo iliwasilisha kesi hiyo ikiungwa mkono rasmi na taifa la Misri ambalo ni mpatanishi katika mzozo huu kati ya Israel na kundi la Hamas, ilisisitiza kuwa operesheni ya Israel inayoendelea huko Rafah inapaswa kutoa msukumo kwa mahakama hiyo ya Umoja wa Mataifa kuchukua hatua mpya za dharura.
Kesi hiyo, ambayo kwa mujibu wa Israel inapaswa kutupiliwa mbali, itaongeza shinikizo la kimataifa linalotaka usitishwaji mapigano na kuachiliwa kwa mateka baada ya zaidi ya miezi saba ya vita.
Wakati huo huo, mwendesha mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC Imran Khan anadhamiria kutoa waranti wa kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Waziri wake wa Ulinzi Yoav Gallant pamoja na viongozi watatu wa Hamas ambao wote hao wanakabiliwa na mashtaka ya uhalifu wa kivita.
Tukio jingine ambalo linachukuliwa kama pigo kwa diplomasia ya Israel, ni uamuzi wa nchi tatu za Ulaya ikiwa ni pamoja na Ireland, Uhispania na Norway, kutangaza mipango ya kuitambua Palestina kama taifa huru.
Israel yaendeleza mashambulizi Gaza
Vikosi vya Israel vimeendeleza mashambulizi ya anga karibu kwenye maeneo yote ya Ukanda wa Gaza. Katika eneo la kaskazini mwa Gaza la Jabalia, ambako mapigano yamepamba moto katika miezi ya hivi karibuni, jeshi la Israel limesema limeipata miili ya mateka watatu baada ya operesheni ya usiku wa kuamkia leo. Jeshi limesisitiza kuwa mateka hao waliuawa wakati wa uvamizi wa Hamas mnamo Oktoba 7.
Wiki iliyopita maiti nyingine nne za mateka zilipatikana kwenye vichuguu huko Jabalia. Daniel Hagari, msemaji wa jeshi la Israel amesema kamwe hawatoacha kupigania uhuru wa mateka waliopo huko Gaza:
“Kuna wanaume, wanawake, watoto na hata watoto wachanga wanaoshikiliwa na Hamas na wanaoishi katika mazingira ya kutisha huko Gaza. Hatutoacha kupigania uhuru wao. Kila nchi inayojielewa duniani ingelifanya hivyo.”
Soma pia: Israel yafanya mashambulizi mabaya katika ukanda wa Gaza
Mapema mwezi huu, Israel ilikaidi miito ya kimataifa na kuanzisha operesheni kamili ya ardhini katika mji wa kusini mwa Gaza wa Rafah. Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa, mashambulizi hayo yamepelekea zaidi ya watu 800,000 kulikimbia eneo hilo.
Katika taarifa iliyotolewa leo Ijumaa, jeshi la Israel limesema wanajeshi wake wanaendelea na operesheni inayoyalenga yale linayosema ni “maeneo ya magaidi” katika mji huo wa kusini, na limedai kufanikiwa kuharibu maghala ya kuhifadhia silaha pamoja na mahandaki.
(Vyanzo: AFP,AP,DPA)