LICHA ya upinzani mkali walionao kutoka kwa Simba SC ya Juma Mgunda, kocha wa Azam FC, Youssouf Dabo anaamini vijana wake wanaweza kupambana katika michezo miwili iliyosalia katika ligi dhidi ya Kagera Sugar na Geita Gold ili kuvuna pointi sita kwa ajili ya kukamilisha mpango wa kupata tiketi ya msimu ujao wa 2024/25 kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kocha huyo raia wa Senegal, amewataka wachezaji wake kuondoa mawazo ya mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Yanga ambao utachezwa Juni 2, Zanzibar na badala yake kuelekeza nguvu zao katika michezo hiyo ili kukamilisha mpango huo.
“Tunatakiwa kuwa makini katika kila mchezo, hesabu zilizopo mbele yetu kwa sasa ni kupata nafasi ya kucheza ligi ya mabingwa msimu ujao, tunaipataje ni kwa kumaliza ligi katika nafasi ya pili, tunajua kuwa Simba nao wapo macho, wanapambana ili kuhakikisha nao wanamaliza msimu katika nafasi hiyo,” alisema na kuongeza;
“Kagera (Sugar) ni miongoni mwa timu shindani katika ligi hivyo hauwezi kuwa mchezo mwepesi hata kidogo, tumejiandaa kukabiliana nao na baada ya hapo tutaelekeza nguvu zetu katika pointi tatu za mwisho ugenini.”
Katika michezo ya mzunguko wa kwanza, Azam iliitandika Kagera Sugar kwenye uwanja wa Kaitaba mvua ya mabao 4-0, Feisal Salum alikuwa mmoja wa wafungaji wa mabao ya timu hiyo, mbele ya Geita Gold vijana hao wa Dabo wakiwa nyumbani kwenye uwanja wao wa nyumbani, Azam Complex waliibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Azam na Simba zinalingana pointi kila mmoja ana 63, wametenganishwa na utofauti wa mabao, matajiri wa Chamazi wapo nafasi ya pili kutokana na kuruhusu kwao idadi ndogo ya mabao 20, Mnyama ameruhusu mabao 25, wababe hao wamefungana idadi ya mabao ya kufunga kila mmoja 56.
Mara ya mwisho kwa Azam FC kushiriki ligi ya Mabingwa Afrika ilikuwa 2015 baada ya kutoka kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara hata hivyo waliishia raundi ya awali kwa kutupwa nje na Al-Merrikh ya Sudan, walipoteza katika michezo yote miwili nyumbani (2-0) na ugenini (3-0).