BENKI ZAJIPANGA KUFUNGUA TAWI MICHEWENI ZANZIBAR

Na. Saidina Msangi, WF, Dodoma.

Serikali imesema kuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetoa idhini kwa Benki ya PBZ kufungua tawi katika eneo la Konde lililopo katika wilaya ya micheweni na matayarisho ya kufungua tawi hilo yanaendelea.

Hayo yameelezwa bungeni, jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), akijibu swali la Mbunge wa Micheweni Mhe. Abdi Hika Mkasha, aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani wa kurejesha huduma za Kibenki za CRDB, NMB na PBZ katika Wilaya ya Micheweni.

Mhe. Chande alisema kuwa Benki za CRDB, NMB na PBZ kwa sasa hazina matawi katika wilaya ya Micheweni ambapo wananchi wa Wilaya ya Micheweni wanapata huduma za kibenki kutoka katika benki hizo kupitia jumla ya mawakala 27 ambapo Benki ya CRDB ina Mawakala 11, NMB 12 na PBZ 4.

‘‘Kabla ya benki kufanya uamuzi wa kufungua tawi jipya, benki husika hufanya upembuzi yakinifu ukiwa na lengo la kuangalia kama kuna uwepo wa biashara ya kutosha ambayo italeta faida kwa benki husika’’ alifafanua Mhe Chande.

Aliongeza kuwa Serikali inatambua ukuaji wa uchumi katika wilaya ya Micheweni na kuwa benki za CRDB, PBZ na NMB zitaendelea kufanya utafiti na upembuzi yakinifu ili kuona uwepo wa tija katika wilaya hiyo ili kuweza kufungua huduma za kibenki.

Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), akijibu swali bungeni jijini Dodoma la Mbunge wa Micheweni, Mhe. Abdi Hika Mkasha, aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani wa kurejesha huduma za Kibenki za CRDB, NMB na PBZ katika Wilaya ya Micheweni Zanzibar.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini – Wizara ya Fedha)

Related Posts