Wasimulia mauaji ya Penina wa Goba

Dar es Salaam. Mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Penina Methody (27) ameuawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali kinachodhaniwa ni panga, chanzo kikidaiwa ni wivu wa mapenzi.

Tukio hilo linalodaiwa kufanywa na mtu anayedaiwa ni mpenzi wake limetokea jana Alhamisi, Mei 23, 2024 Goba Centre, Wilaya ya Kinondoni anapofanyia biashara zake Penina.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema leo Ijumaa Mei 24 2024 kuwa watatoa taarifa kamili kuhusu tukio hilo.

Akisimulia tukio hilo mmoja wa bodaboda aliyekuwa akimbeba Penina amesema siku nne kabla ya kuuawa, Penina na mwanamume mmoja walipigana kwa kurushiana chupa.

“Kabla ya jana walipigana hapa baa wakarushiana chupa za kutosha kwa kuwa ni wapenzi wakamalizana tofauti zao na kwenda nyumbani kwao,” amesema boda huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Eneo yalipofanyika mauaji ya mfanyabiashara, Penina Methody anayedaiwa kuuliwa na na mpenzi wake kwa kumkata kwa panga.

Amedai kuwa mtu huyo alishamkataza Penina kufanya biashara ya duka la pombe licha ya kuchangia kiasi cha pesa cha kufungua biashara hiyo na alimtaka ashinde nyumbani kwa kuwa alishaweka wasaidizi wanne wa kumsaidia biashara hiy, hivyo alimtaka awe anachukua mahesabu na kurudi nyumbani.

Alfajiri ya kuamkia Mei 23, 2024 mwanamume huyo alikodi bodaboda na kufika eneo la tukio, alimkuta Penina akiwa anarudi nyumbani baada ya kufunga biashara.

“Mwanamume alishamkataza asiwe anakuja katika hii biashara na kukesha baada ya kuona hajarudi nyumbani akaamua kumfuata ofisini kwake na alipofika alitoa panga na kuanza kumkata kata,” amesema.

Amesema kwa kuwa kilikuwa kitendo cha haraka bodaboda aliyembeba mwanamume huyo alishuka na kukimbilia Kituo cha Polisi cha Goba akifikiri panga lile lilitolewa kwa ajili yake, waliporejea walikuta tukio limemalizika.

“Baada ya kufanya unyama wake anawaambia watu haamini kama ameua, hivyo alitaka watu wamuangalie mara mbili kwa kuwa haikuwa dhamira yake kumuua mpenzi wake,” amesema.

Mama mdogo wa marehemu Ziada Mnyoo amesema tangu wamfahamu mwanamume huyo hawajawahi kusikia kuwa wana ugomvi, hivyo kwao limekuwa jambo la kushtukiza.

“Sijui kitu gani kimetokea maana hatujawahi kusikia wala kuwaona wakigombana maana walikuwa wanapendana hadi sasa sababu ya kufanywa kwa tukio hilo hatuelewi chanzo ni nini,” amedai Ziada.

Amedai kuwa marehemu ameacha watoto wawili mmoja wa miaka 10 na mwingine wa miaka mitano.

Penina anatarajiwa kuzikwa leo Mei 24, 2024  saa 10 jioni katika makaburi ya kwa Awadhi.
 

Related Posts