Dar/mikoani. Wakati msimu wa mvua ukimalizika ukitajwa kuwa chanzo cha baadhi ya bidhaa za mbogamboga kupanda bei sokoni, kumeibuka sababu mpya madalali na walanguzi wa mbolea wakitajwa.
Ingawa baadhi ya bidhaa za viungo na mbogamboga zimeanza kushuka bei, wachuuzi wanasema walanguzi wa mbolea na madalali wasipodhibitiwa hali inaweza kuwa mbaya.
Katika masoko yaliyofikiwa na Mwananchi mkoani Dar es Salaam na baadhi ya mikoani, wachuuzi wanaeleza bei ya bidhaa imeshuka kidogo chanzo ni madalali waliopo shambani.
Mfanyabiashara sokoni Ilala mkoani Dar es Salaam, Rose Siara anasema: “Tunapata wakati mgumu baada ya madalali kuhamia mashambani, wananunua mazao kwa wakulima kwa gharama ndogo lakini wanatuuzia kwa bei mara mbili ya waliyonunulia.”
Amesema Mei 21, 2024 alinunua nyanya chungu kutoka Dumila mkoani Morogoro kwa Sh55,000 kwa gunia lenye ndoo 10, pamoja na nauli ya kusafirisha mzigo ambapo amelazimika kuliuza Sh60,000 ili kupata faida ya Sh5,000.
Gunia hilo anasema kabla ya mvua na madalali kuhamisha shambani walikuwa wakinunua kati ya Sh20,000 na Sh25,000.
Gunia la mboga za majaji kutoka mkoani Morogoro sokoni hapo linauzwa kati ya Sh100,000 na Sh120,000 kabla ya msimu wa mvua liliuzwa Sh80,000.
Kwa bei ya rejareja anasema kulingana na aina ya mboga, fungu moja linauzwa kati ya Sh700 hadi Sh1,500, kutoka Sh500 ya awali.
Siara ambaye ni dalali sokoni hapo amesema vitunguu maji vimeshuka bei kiasi kidogo, ambapo kilo moja ikiuzwa kati ya Sh5,000 hadi Sh6,000, huku bei ya jumla ikiwa Sh500,000 hadi Sh800,000 kwa gunia. Awali gunia liliuzwa Sh300,000 na kati ya Sh800 hadi Sh1,500 kwa kilo.
Mfanyabiashara katika soko la Buguruni, Ally Kiungo anasema baada ya mvua kukoma, gunia la pilipili hoho limeshuka bei kutoka Sh230,000 hadi Sh140,000.
“Nauza hoho na bamia, kwa sasa zimeshuka bei kidogo lakini tunapofuata mzigo tunapata wakati mgumu kwa sababu ya wasimamizi mashambani. Tunanunua bidhaa kwa bei kubwa, kwa mfano gunia la bamia la ndoo 10 liliuzwa Sh230,000 hivi sasa limeshuka kidogo ni Sh150,000,” anasema.
Vitunguu swaumu havishikiki
Mkoani Dar es Salaam kilo ya vitunguu saumu ni Sh20,000 kwa bei ya jumla na rejareja ni Sh25,000.
John Beda, mkulima wilayani Babati mkoani Manyara anasema msimu uliopita vitunguu saumu viliuzwa Sh2,500 hadi Sh3,000 kwa kilo lakini sasa ni Sh10,000 hadi Sh15,000 kulingana na eneo.
“Mvua zilikuwa nyingi maji yakatuama na kusababisha wakulima kushindwa kupanda kitunguu saumu kwa wakati ndiyo sababu bei imepanda maana waliovuna kwa wingi ni wachache,” anasema.
Mfanyabiashara katika Soko la Kibandamaiti, Mkoa wa Mjini Magharibi, Salumu Mohammed anasema kilo moja ya vitunguu vyenye ubora wananunua Sh15,000 na wao wanauza kati ya Sh20,000 hadi Sh22,000.
Mkazi huyo wa Zanzibar anasema awali walinunua Sh7,000 na kuuza Sh10,000 kwa kilo, lakini sasa vile ambavyo havina ubora wanauziwa Sh10,000 hadi Sh12,000 kwa kilo.
“Hali ya uingiaji wa vitunguu saumu hairidhishi ndiyo maana bei imekuwa juu, hata wasambazaji wanachukua kwa bei kubwa huko Tanzania Bara,” anasema Shawwal Abdulrahman Takadiri, ambaye ni mkuu wa soko hilo.
Wafanyabiashara wa kabichi katika Soko la Kigogo wanasema bei imepungua kidogo baada ya msimu wa mvua. Bei ya jumla amesema wanauza kati ya Sh250,000 na Sh300,000, huku rejareja ni Sh2,500 hadi Sh3,000.
Mfanyabiashara wa kabichi, Maria Idifonsi anasema: “Mvua zimekata lakini kupata kabichi ya Sh500 kama zamani inategemea na ubora ambao mtu amenunua.”
Halima Hanzuruni, mfanyabiashara sokoni Ilala anasema ili kuepuka upandaji wa gharama za bidhaa zinazolimwa pembezoni mwa mito, Serikali iwapatie wakulima eneo ambalo halitaathiriwa na mvua.
“Mkoa wa Dar es Salaam kwa upande wa mboga unalishwa na Morogoro ambao ulikumbwa na maji mengi kipindi cha mvua, hivyo Serikali ifikirie namna inaweza kuwasaidia wakulima ili kusiwe na changamoto kwenye vyakula,” anasema.
Anasema uboreshwaji wa miundombinu ya mashamba utasaidia bidhaa kutopanda bei kwani hivi sasa magari yanashindwa kufuata bidhaa kutokana na barabara kuharibika. Hali hiyo pia husababisha baadhi ya mazao kuharibika yakiwa shambani.
Kwa mujibu wa wafanyabiashara, wakulima wamekuwa wakilalamika kutumia gharama kubwa katika uzalishaji, huku kukiwa na ulanguzi wa mbolea.
Mkulima wa mbogamboga mkoani Morogoro, Upendo Kilonzo anasema upatikanaji wa mbolea ni mgumu kwa sababu bila kuwa na kitambulisho cha Taifa huwezi kupatiwa.
“Sisi wakulima tumepata wakati mgumu wa kupata mbolea ndiyo maana tunauziwa kwa bei ya juu hususani kama huna kitambulisho cha Nida,” anasema Upendo.
Anasema mbolea inapatikana kwa gharama ya kati ya Sh45,000 hadi Sh70,000 kwa mfuko.
Akilizungumzia hilo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweri anasema kumekuwa na walanguzi kwenye uuzaji wa mbolea na tayari wameshawachukulia hatua kwa kuwapeleka mahakamani.
Anatoa mfano wa wauzaji mkoani Songwe ambako wamechukuliwa hatua, akiwataka wakulima kutoa taarifa wanapokutana na changamoto ya aina hiyo.
“Kila siku tumekuwa tukitoa taarifa ili kupambana na walanguzi na tunasema kabisa kama mbolea inauzwa Sh70,000 na mkulima akauziwa Sh72,000 anatakiwa kupiga simu muda wote,” anasema.
Kuhusu upatikanaji wa mbolea kwa wakati anasema ipo na kama kuna malalamiko itakuwa muhusika yupo mbali na maduka inakouzwa bidhaa hiyo.
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe akiwasilisha hotuba ya bajeti bungeni hivi karibuni alisema katika kurahisisha usambazaji wa mbolea kwa wakulima, wizara imeongeza idadi ya waingizaji wakubwa wa bidhaa hiyo kutoka 28 mwaka 2022/2023 hadi 31 mwaka 2023/2024; mawakala wadogo 3,265 mwaka 2022/2023 hadi 3,500 mwaka 2023/2024.
Alisema wamesajili vyama vya ushirika 776 kwa ajili ya kuwa mawakala wa kusambaza mbolea, pia maghala 987 yenye uwezo wa kuhifadhi tani 458,610 yameainishwa nchini kwa ajili ya kuhifadhi mbolea.
“Wizara katika mwaka 2024/2025 itaendelea kutoa ruzuku ya mbolea na viuatilifu kupitia mpango wa ruzuku kwa mazao yote. Hivyo, kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Serikali itaratibu uingizwaji wa tani 1,086,115 za mbolea na kuzisambaza kwa wakulima kwa mpango wa ruzuku utakaoendelea hadi mwaka 2025/2026,” alisema.
Bashe alisema wizara itakamilisha vigezo muhimu katika mfumo wa usajili wa wakulima; na itasajili wakulima, waagizaji na wasambazaji wa mbolea katika mfumo wa kielektroniki kwa lengo la kuimarisha usambazaji wake nchini.
Imeandikwa na Devotha Kihwelo na Glorian Sulle (Dar), Joseph Lyimo (Manyara), na Zuleikha Fatawi (Zanzibar)