Nabi amshauri Aziz Ki, akimtaja Mayele

KOCHA wa zamani Yanga, Nasreddine Nabi amemshauri kinara wa mabao na kiungo mshambuliaji wa mabingwa hao wa Tanzania, StephaneAziz Ki juu ya mipango ya kuondoka klabuni hapo akikumbushia ishu ya Fiston Mayele aliyepo Pyramids ya Misri kwa sasa.

Kumekuwapo kwa tetesi kwamba Aziz KI hajasaini mkataba huku akitakiwa na klabu kadhaa zikiwamo mbili za Afrika Kusini, jambo linalowafanya mabosi wa Yanga kuhaha kumbakisha nyota huyo.

Hata hivyo, Nabi anayeifundisha FAR Rabat kwa sasa aliyewahi kumfundisha kiungo huyo msimu uliopita akiwa Jangwani ambapo Aziz Ki hakuwa mzuri kwake tofauti na ilivyo sasa akiwa ameshaifungia mabao 17 na kuongoza orodha ya wafungaji wa Ligi Kuu Bara, ameliambia Mwanaspoti kuwa kiwango cha mchezaji huyo kimeongezeka zaidi msimu huu kuliko uliopita.

Amesema anaelewa kwamba ni lazima kutakuwa na ofa nyingi  kwa mchezaji huyo kwa vile mkataba alionao Yanga unamalizika na kiwango chake ndicho kimezidi kuwa bora, lakini anatakiwa atulize akili asiharakishe kuondoka kwa sababu ya fedha.

“Anaweza kuona na kujifunza kupitia Mayele, ambaye bado anajitafuta Misri tangu alipotoka Yanga sio rahisi mchezaji akitoka na kwenda ligi kubwa zaidi, kisha akafanikiwa haraka au kuendeleza kasi yake,” amesema Nabi na kuongeza: 

“Akibaki Yanga kwa mwaka mmoja au miaka miwili zaidi kisha akaendeleza kiwango hiki atakuwa amekomaa zaidi kwa kuwa ligi ya Tanzania ni ngumu na inaendelea kukua na kufahamika kwa ukubwa.”

Akiwa chini ya Nabi, kiungo huyo raia wa Burkina Faso, alifunga mabao tisa tu msimu uliopita, huku Mayele akimaliza kinara wa Ligi Kuu sambamba na Saido Ntibazonkiza kila mmoja akifunga mabao 17 ambayo yameshafikiwa na Aziz Ki na jioni ya kesho anatarajiwa kushuka uwanjani kuivaa Tabora United, kesho.

Kama atafunga bao, litamfanya apiku rekodi hiyo ya Mayele na Saido kwa msimu uliopita, lakini akizidi kujiweka pazuri kutwaa kiatu cha dhahabu akichuana na Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam mwenye mabao 16 na ambaye jioni ya kesho atakuwa pia uwanjani kuikabili Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Related Posts