Majeruhi mlipuko wa Mtibwa wafariki dunia, vifo vyafikia 13

Morogoro. Idadi ya watu waliofariki dunia baada ya kupasuka bomba la kusafirisha mvuke wa joto kwenye kiwanda cha kuzalisha sukari cha Mtibwa Mvomero mkoani hapa, imeongezeka na kufikia 13.

Majeruhi hao waliokuwa wakitibiwa  Hospitali ya Benjamini Mkapa Dodoma baada ya kupatiwa rufaa jana kutoka Hospitali ya Turiani, wamefariki dunia.

Akizungumza kwa njia ya simu na Mwananchi Digital leo Ijumaa Mei 24, 2024, Daktari wa magonjwa ya dharura wa Hospitali ya Benjamini Mkapa, George Dilunga amesema majeruhi wamefariki kwa nyakati tofauti.

“Majeruhi hawa tuliwapokea jana wakitokea Hospitali ya Turiani Morogoro, walidhurika baada ya kuunguzwa na mvuke wa Kiwanda cha Mtibwa Sukari, mmoja kati yao alifariki muda mchache baada ya kufikishwa hapa hospitali, kijumla hali zao zilikuwa mbaya sana na mwingine baada ya kuona hali imebadilika, tulimuhamishia kitengo cha uangalizi maalumu (ICU) na amefariki dunia alfajiri ya leo, hivyo wote walioletwa hapa wamefariki dunia,” amesema Dk Dilunga.

Amesema hospitalini hapo walisindikizwa na wauguzi wasaidizi kutoka Hospitali ya Wilaya ya Mvomero kule Turiani na hawakuja na ndugu zao.

Hata hivyo, Dk Dilunga amesema marehemu George Barnaba na Michael Kadudu, walikuwa wameungua sehemu mbalimbali za miili yao, ikiwamo usoni, mikono, miguu, tumboni na majeraha yalikuwa makubwa kwa kuwa moto uliingia ndani zaidi.

Mwananchi Digital imemtafuta Meneja wa Kiwanda cha Sukari Mtibwa, Moses Tenda ili kujua kama wamepata taarifa za vifo hivyo, amesema bado hawajapokea taarifa hiyo.

“Ila ni kweli jana kuna majeruhi wawili walisafirishwa kwenda Hospitali ya Benjamini Mkapa kwa ajili ya matibabu, lakini mpaka sasa sijapata taarifa kama wamefariki dunia acha nifuatilie,” amesema meneja huyo na kuongeza;

“Kwa sasa bado nina kikao na watu wa Osha, naomba unipe muda ili nifuatilie kujua ukweli kisha nitakurejea kukupa taarifa rasmi,” amesema Moses.

Jana alfajiri wakati wakijiandaa kuanza uzalishaji kiwandani hapo, bomba  linalopokea mvuke wenye joto kali linalofikia nyuzi joto 420 lililipuka na kuwaathiri waliokuwa kwenye chumba cha uendeshaji mitambo.

Meneja wa umeme katika kiwanda hicho, Juma Balanda alisema ilitokea hitilafu iliyosababisha bomba hilo kulipuka.

“Ajali imetokea baada ya bomba la kupokea mvuke wa joto linalofikia nyuzi  450 kupasuka na lile joto kuwazidi wale watumishi na kufariki dunia.

“Awali, tulikuwa na shughuli ya maboresho kwenye mitambo yetu kwenye mfumo wa kusafirisha joto, hivyo kabla ya kuanza uzalishaji rasmi, ndio ukatokea mpasuko ambao umeleta madhara haya.”

Alisema chumba kilikuwa na wataalamu  16, mmoja simu iliita akatoka kwenda kuisikiliza na huko nje akakutana na mtumishi mwingine naye alikuwa akizungumza na simu, wakanusurika.

Related Posts