Dar es Salaam. Katika kukabiliana na mahitaji ya afya ya akili ambayo mara nyingi hayazingatiwi shuleni nchini, Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU) kimechukua hatua ya kukuza utamaduni wa ustawi wa akili kuanzia ngazi ya chini ya elimu.
Hivi karibuni AKU kiliandaa semina iliyowakutanisha wanafunzi wa shule za sekondari na walezi, lengo kuu likiwa ni kuongeza uelewa kuhusu afya ya akili na usimamizi wa mfadhaiko.
Baada ya kufanya hivyo, kwenye shule kadhaa jijini hapa, katika kuongeza wigo wa mafunzo hayo, AKU kiliendesha mafunzo hayo wilayani Kisarawe mkoani Pwani kwa kukutana na wanafunzi wa kidato tano na kidato cha sita katika shule za sekondari za Minaki na Jokate Mwegelo.
Mtaalamu wa afya ya akili na mhadhiri katika Shule ya Uuguzi na Ukunga ya AKU, Dk Stewart Mbelwa, amesisitiza umuhimu wa kushughulikia masuala ya afya ya akili miongoni mwa wanafunzi, hasa wakati wanapochagua masomo yanayoainisha kazi zao za baadaye.
Dk Mbelwa amesema changamoto ya mfadhaiko imezidi kuwa kubwa wanafunzi wakati huu, akisisitiza umuhimu wa huduma za ushauri nasaha kuwasaidia kusimamia changamoto hizi kwa ufanisi.
“Kila hatua ya maisha ya mwanafunzi kuna mfadhaiko, lakini kundi hili mara nyingi halizingatiwi linapokuja suala la kulinda afya yao ya akili. AKU imejitolea kuwawezesha wanafunzi ngazi ya msingi kushughulikia changamoto hizi na kuhakikisha kuwa hazizuii maendeleo yao ya kitaaluma au kuwanyima haki yao ya elimu,”
Amewahimiza vijana kuhusu njia bora za kusimamia mfadhaiko, hasa wakati wa mitihani ambayo haizingatii hali ya mwanafunzi katika mambo mengine ya kijamii kwa wakati huo.
Amedai kuwa matatizo ya afya ya akili miongoni mwa wanafunzi yamekuwa yakiongezeka, ingawa mara nyingi yanabaki pembeni katika majadiliano na mipango inayolenga ustawi wa akili.
Dk Mbelwa amesisitiza umuhimu wa dharura ya kushughulikia suala hili, hasa katika shule za umma ambapo wanafunzi kutoka mazingira duni wanakabiliana na changamoto nyingi kuanzia masuala ya kifamilia hadi ugumu wa kiuchumi.
Mhadhiri wa Shule ya Uuguzi na Ukunga ya AKU, Elianeth Kiteni amewahimiza wanafunzi kujijua wenyewe na kuepuka hali yoyote inayoweza kuathiri kujifunza kwao shuleni na kuwataka kuchagua vyuo vizuri vitakavyowasaidia kufikia ndoto zao.
Makamu mkuu wa Shule ya Minaki, Anabela Sanga, amesema hawakutarajia ziara kutoka katika chuo kikuu chenye heshima kama AKU, akikishukuru kwa hatua hiyo ya kuwajengea uwezo.
“Mmefika wakati mwafaka ambapo wanafunzi wetu wanakaribia kumaliza kidato cha tano na sita, walikuwa hawajapata habari kama hii, hasa kutoka kwa wataalamu kama nyinyi, hii ni faida kubwa kwetu,” amesema.
Mmoja wa wanafunzi wa Minaki, Denis Mburi alisema: “Nina furaha kutokana na ushauri na mwongozo nilioupata kutoka kwa wataalamu wa AKU. Sikujua wangeweza kutunyenyekea na kuja kutujengea uwezo.
“Aina ya mfadhaiko tunayopata wakati mwingine tunapambana nayo, lakini leo tumeelewa umuhimu wa kuepuka mafadhaiko, hasa tunapokuwa shuleni.”